Rais Mwinyi: Tuendelee kuhubiri Amani katika jamii

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema suala la kuhubiri Amani sio la kuachiwa Viongozi wa dini pekee bali kwa makundi mbalimbali ya kijamii yana wajibu wa kulipa mkazo suala hilo.

Ameyasema hayo leo Oktoba 4, 2024 alipojumuika na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika sala ya Ijumaa na Maulidi ya Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) na yaliofanyika Msikiti wa Taqwa Bweleo ,Wilaya ya Magharibi B .

Aidha Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa makundi matatu ya kijamii yana nguvu kubwa ya kuhimiza Amani ya nchi endapo yatadhamiria kuhubiri Amani katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Ameyataja makundi hayo kuwa Wanasiasa, Waandishi wa Habari na Viongozi wa dini na kuyataka kutimiza wajibu wao.

Halikadhalika amesisitiza kuwa hakuna jambo litakaloshindikana endapo nchi itakuwa katika Amani ,Umoja na Upendo miongoni mwa wananchi .

Akizungumzia maadili amewasisitiza Waumini wa Kiislamu kuyaishi maisha ya Mtume Muhammad kwa Vitendo kwa kufuata miongozo na maelekezo yake ili kuwa na jamii bora 

Related Posts