Na: Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Idara ya Kazi, imetoa elimu ya sheria za kazi kwa Wafanyakazi na Waajiri wa sekta za ulinzi Jijini Dar es salaam.
Akizungumza Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa amesema kuwa dhumuni la semina hiyo ni kutoa Elimu ya Sheria za Kazi katika Sekta ya Ulinzi nchini ili kuendelea kupunguza changamoto zinazowakabili baadhi ya wafanyakazi katika Sekta hiyo
Aidha, Mkangwa amebainisha baadhi ya malalamiko ambayo yamekuwa yakiripotiwa Idara ya kazi ikiwemo wafanyakazi kuajiriwa bila mikataba, Waajiri kutowasilisha michango katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kuachishwa kazi kiholela bila kuzingatia sheria za kazi.
“Ni matumaini yangu semina hii itakwenda kuondoa changamoto za ukiukwaji wa sheria za kazi ambazo zimekuwa zikiripotiwa ofisini mara kwa mara” amesema.
Awali akizungumza Afisa Matekelezo kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Asha Udindo ametoa rai kwa Waajiri wa sekta hizo kujiunga WCF na kuwasilisha michango kwa wakati ili kulinda haki zao dhidi ya majanga yanayoweza kuwapata wafanyakazi wao wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kila siku.
Naye, Meneja Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Dar es salaam Feruzi Mtika amesema Serikali haitawavumilia waajiri wote wa sekta binafsi ambao wanakata michango ya wafanyakazi wao bila kuiwasilisha katika Mfuko huo.