ALAF Yazindua Jogging Club Kuimarisha Afya Ya Wafanyakazi

AFISA Mtendahji Mkuu wa ALAF Limited, Ashish Mistry (mwenye miwani) akiongoza wafanyakazi wa kampuni hiyo katika kufanya mazoezi ya kunyoosha viungo (aerobics) wakati wa uzinduzi wa ALAF Jogging Club kiwandani hapo Jumamosi.

KATIKA hali ya kuhakikisha wafanyakazi wanazalisha kwa ufanisi zaidi, ALAF Limited Tanzania imezindua ALAF Jogging Club ambayo pamoja na mambo mengine itahakikisha wafanyakazi wanazingatia mazoezi kwa afya njema.

Akizindua Club hiyo, Afisa Mtendahji Mkuu wa ALAF Limited, Ashish Mistry, alisema hatua hii itasaidia kukuza afya ya mwili na akili miongoni mwa wafanyakazi wa kampuni hiyo wanapokuwa kazini lakini pia katika maisha yao majumbani.

“Unapokuwa na afya nzuri ya mwili na akili, hata uzalishaji unakuwa bora zaidi ndio maana tunasisitiza kuhusu mazoezi ya mara kwa mara kwa wafanyakazi wetu,” alisisitiza Bw. Mistry.

Alisema uongozi wa kampuni hiyo utaendelea kushirikiana na wafanyakazi kuhakikisha mikakati kama hii yenye manufaa kwao inafanikiwa huku akishiriki katika mazoezi ya kunyoosha viungo wakati akizindua club hiyo kiwandani hapo mwishoni mwa wiki.

Naye Meneja Rasilimali watu wa Alaf Limited, Jumbe Njero allielezea kuwa club hiyo itawezesha wafanyakazi kuwa mahiri katika afya.

“Tunafahamu kuwa tunajenga nyumba na nyumba hizi lazima ziendane na watu wenye afya bora. Huwezi kujenga kwa miaka 50 halafu wewe mwenyewe unakaa kwa miaka mitatu tu,” alishauri.

Alitoa wito kwa wafanyakazi wote watoe kipaumbele kwenye suala la mazoezi na kujitengea muda ili wapate mafanikio katika azma hii ya kukuza afya ya mwili na akili.

Meneja Uzalishaji ambaye pia ni mratibu wa masuala ya michezo kiwandani hapo, Aman Kitale, alisema mazoezi yatawasaidia wafanyakazi kuongeza ufanisi na kuzalisha bidhaa ambazo zinaendana na soko.

Alisema wafanyakazi walianza kwa kukimbia kilomita 15 kutoka kiwandani hadi Uwanja wa Taifa na kurudi kiwandani ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa club hiyo.

“Tumefanya jogging kuanzia saa kumi na mbili kamili hadi saa moja asubuhi kutoka ALAF hadi Uwanja wa Taifa na kurudi, tumefanya aerobics hapa canteen huku lengo kubwa likiwa ni kuimarisha afya za wafanyakazi.

ALAF Limited ni kampuni inayoongoza nchini Tanzania kwa kutengeneza mabati ya kuezekea nyumba. Ni kampuni iliyoanzishwa mwaka 1960, na inaendelea kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.

ALAF imeunganisha kikamilifu operesheni, si tu kwa kutengeneza mabati, lakini pia kwa kuzalisha vifaa vinavyotumika katika shughuli mbalimbali za uezekaji wa nyumba. ALAF Limited hutengeneza vifaa mbalimbali vya metali kwa matumizi mbalimbali ya uezekaji wa nyumba.

Related Posts