DUWASA WAANZA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA KWA KISHINDO, WAFANYAKAZI WASISITIZWA KUWAHUDUMIA WATEJA KWA UPENDO

Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Dodoma(DUWASA) Mhandisi Aron Joseph amesisitiza Watumishi kuendelea kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyapatia ufumbuzi.

Mhandisi Aron ameyasema hayo leo Oktoba 7,2024 jijini Dodoma wakati akizundua wiki ya huduma kwa wateja.

Amesema wananchi wanapokuwa na malalamiko wanataka kupewa ufafanuzi Ili kuondoa sintofahamu.

“Tukiwa katika wiki ya huduma kwa wateja niendelee kuwasihi ndugu zangu mjikite katika kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyapatia ufumbuzi Ili kuendelea kuboresha huduma zetu,”amesema Mhandisi Aron

Katika hatua nyingine Mhandisi Aron amesema katika kipindi hicho watafanya kazi ya kuwafikia wateja na kusikiliza kero zao na kuzitatu.

Kwa upande wake Mtumishi wa DUWASA Winifrida Kulanda amesema katika wiki ya huduma kwa wateja ni muhimu kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na matumizi sahihi.

Amesema pia wananchi waendelee kuelimishwa kuhusu athari za uvujaji na upotevu wa maji hasa ikizingatiwa kwasasa ongezeko la watu kwa Mkoa wa Dodoma linakuwa Kwa Kasi.

“Tunaendelea kuhamasishana sisi kwa sisi kulipa maji kwa wakati lakini pia kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu faida za kutunza vyanzo vya maji na kuepuka upotevu wa maji,”amesema Kulanda

Naye Ofisa Ankara na Takwimu DUWASA Venancy Kuhumbi amesema katika wiki ya huduma kwa wateja wamejipanga kuwafuata wateja na kusikiliza kero zao na kuangalia njia bora ya kuzitatua.

Amesema huduma ya maji ni muhimu na haina mbadala hivyo ili kuondoa sintofahamu na maswali kwa wananchi lazima kuwasikiliza na kuwatolea ufafanua wa changamoto zao.

“Wiki hii ni muhimu kwetu kwa sababu tumejipanga kuwafikia wateja wetu pamoja na kuangalia changamoto zao ambazo zinawakabili na kuzitatua ,”amesema Kuhumbi




Related Posts