Maandamano ya kumbukumbu ya mashambulizi ya Oktoba 7 – DW – 07.10.2024

Maandamano ya kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja ya mashambulizi ya Oktoba 7 dhidi ya Israel na vita katika ukanda wa Gaza yamefanyika mjini Berlin, Düsseldorf, Hamburg na Munich huku moja kati ya maandamano hayo yakishuhudia ghasia.

Polisi walishika doria ili kuhakikisha maandamano hayo yanafanyika kwa njia ya amani, japo yaligeuka na kuwa ya vurugu mjini Berlin wakati waandamanaji wanayoiunga mkono Palestine walipowarushia polisi mawe na chupa.

Polisi imesema takriban watu 3,500 walishiriki maandamano hayo mjini Berlin japo baadhi walijaribu kuvuruga amani na kuwashaka fashifashi.

Soma pia: Israel yashambulia vikali Hezbollah mjini Beirut

Katika eneo la Kreuzberg, polisi iliwatahadharisha watu waliokuwa wakishiriki maandamano hayo kuwa, “usalama wa umma uko hatarini,” na kuongeza kuwa visa vya uvunjaji wa sheria vilikuwa vinafanywa na watu waliokuwa miongoni mwa waandamanaji hao.

Takriban watu 3,500 walishiriki katika maandamano yalioandaliwa chini ya kauli mbiu “maandamano dhidi ya mauaji ya halaiki katika ukanda wa Gaza,” idadi hiyo ikiwa zaidi ya watu 1,000 ambao awali walijiandikisha kushiriki.

Polisi yakabiliana na waandamanaji waliozua vurugu

Berlin | Maandamano | Palestine
Maafisa wa polisi mjini Berlin wakikabiliana na waandamanaji wakati wa maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina Picha: Christian Mang/REUTERS

Maandamano hayo yalitarajiwa kuvutia watu wapatao 1,000 na yalianza katika wilaya ya Kreuzberg kabla ya kuelekea eneo la Neukölln, lenye idadi kubwa ya watu wa jamii ya Kiarabu.

Maandamano tofauti ya kuiunga mkono Israel yaliyopewa jina “pamoja dhidi ya uhalifu wa Hamas kwa raia wa Israel na Wapalestina na kwa ukombozi wa mateka na kumaliza utawala wa Hamas katika ukanda wa Gaza,” yalitarajiwa kuvutia watu 500 katika eneo la kati la Mitte, mjini Berlin.

Soma pia: Ayatullah Ali Khamenei atetea kuishambulia Israel

Mzozo ulioanza wakati wapiganaji wa kundi la Hamas walipoivamia ardhi ya Israel mnamo Oktoba 7, mwaka 2023 na kuwaua takriban watu 1,2000 na kuwachukua mateka watu 250, utakuwa unatimiza mwaka mmoja leo Jumatatu.

Israel ilijibu kwa kufanya mashambulizi makubwa katika ukanda wa Gaza ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 41,800 kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

Wizara hiyo ya afya haitofautishi kati ya vifo vya wapiganaji wa Hamas na raia wa kawaida. Takwimu hizo haziwezi kuthibitishwa kwa njia huru.

 

Related Posts