Madaktari Bingwa wa Rais Samia wapatao 57 wamepokelewa mkoani Tabora na Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt.Rogath Mboya, ambapo watafanya kazi ya kutoa huduma za Kibingwa kwa siku sita sambamba na kuwajengea uwezo wataalam watakao wakuta kwenye vituo.
Akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi Oktoba 07, 2024 Katibu Tawala huyo amewataka Madaktari hao kwenda kuwahudumia wananchi wa Tabora kwa moyo wa upendo ili waendelee kukumbukwa hata watakapo ondoka.
“Najua mtakuwa mkoani kwetu kwa siku sita kuanzia leo, na tayari mkoa tumefanya maandalizi yote muhimu, ikiwepo kuwatangazia wananchi kwenye maeneo yote yenye mikusanyiko kama Nyumba za Ibada, Masokonj, Minada lakini pia magari ya matangazo yaliopita kwenye maeneo yote ya mkoa wetu katika Halmashauri zote Nane”. Amesema Mboya
Katibu Tawala huyo ametumia fursa hiyo kumshuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia mkoa huo kupokea zaidi ya Bilioni 29.3 zilizoelekezwa kwenye uimarishaji wa miundombinu ya Afya na vifaa tiba.
“Ujio wenu unazidi kutuonesha ni jinsi gani Mhe. Rais anatupenda maana baada yakutuimarishia miundombinu ameamua kutushushia huduma hadi ngazi ya za msingi, nani kama mama?.” Amesema Katibu Tawala Mboya
Mboya pia amewataka watumishi wa Afya katika mkoa huo na wananchi kwa jumla kuwapa ushirikiano Madaktari Bingwa waliopangwa kwenye mkoa wao.
Akitoa Salaam za Wizara Mkurugenzi wa Afya ya uzazi kwa huduma za mama na mtoto Dkt. Felix Bundala amesema zoezi hilo linafanyika ikiwa ni matokeo ya mafanikio ya awamu ya kwanza.
“Takribani ni wananchi 70,000 walifikiwa na huduma hizi za Kibingwa awamu ya kwanza, huku ikadiriwa kupunguza gharama hadi kufikia kiasi cha shilingi elfu 20 kwa kila mtu aliyehudumiwa, hivyo Mhe. Rais akaona ni vema turudie tena zoezi ambalo tutafika kwenye Halmashauri zote 184 kama awali.” Amesema Dkt. Bundala.
Akiongea kwa niaba ya Waganga Wakuu wote wa wilaya za mkoa huo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Kaliuwa Dkt. Irene Napina Amesema wamefanya uhamasishaji kwenye maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu ikiwepo nyumba za Ibada na kuwaomba wananchi kujitokeza.
Wakati wa kambi hiyo Madaktari hao watahudumia Magonjwa ya ndani, Watoto, wanawake, kinywa na meno, Upasuaji, utaalamu wa usingizi na ganzi salama, upasuaji wa njia ya mkojo, mifupa pamoja na kutoa huduma za Uuguzi na wakunga Bobezi.