Miaka 60 ya Ruaha yashusha neema kwa wenye uhitaji maalum kata ya Dodi

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini Mhe. Kheri James amekabidhi msaada wa vifaa na mahitaji wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 7.6 uliotolewa na Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa ajili ya wananchi wenye mahitaji maalumu wa vijiji vya Kata ya Idodi iliyoko wilaya ya Iringa vijijini.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo katika kijiji cha Tungamalenga ikiwa ni mwendelezo wa wiki ya Maaadhimisho ya miaka 60 ya hifadhi hiyo yanayotarajia kufikia kilele chake Oktoba 07, 2024.

Vifaa vilivyotolewa kwa wananchi hao ni pamoja na viti vinne vya magurudumu kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalumu, viatu jozi 44 kwa wanafunzi wa kike na kiume wa Shule za Msingi za kata hiyo, mashati ya shule 44, kaptula kwa wanafunzi wa kiume 21, sketi kwa wanafunzi wa kike 23, mafuta ya kupikia ya lita 10 ndoo 20, sabuni boksi 20 na Unga mifuko 20 yenye ujazo wa kilogramu 50 kila moja.

Akikabidhi vifaa hivyo, Mhe. James alisema, “Lengo la hafla hii ni kushiriki mafanikio ya miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa Ruaha tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964. Ni dhahiri kuwa kuwepo kwa hifadhi hii ni matokeo ya juhudi zenu za kushirikiana na wahifadhi hawa kuzilinda rasilimali hizi.”

Naye, Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini – TANAPA, Naibu Kamishna Steria Ndaga alisema, “Hifadhi ya Taifa Ruaha inazungukwa na vijiji 84 kutoka wilaya za Iringa, Mufindi, Mbarali, Chunya na Chamwino ambavyo vimeendelea kunufaika na miradi mbalimbali ya kijamii kwa nyakati tofauti. Lengo la kufanya hivyo ni wananchi wajue umuhimu na thamani ya maliasili zinazowazunguka ili wazitunze kwa faida yao na taifa kwa ujumla.”

Hata hivyo, Kamishna Ndaga aliongeza kuwa kupitia Mpango wa Ujirani Mwema wananchi hupewa elimu ya uhifadhi na ujasiriamali. Vilevile, hifadhi imeshiriki kufadhili miradi mbalimbali ya ujenzi wa shule, zahanati, visima vya maji safi na salama, mabweni na vyoo kwa ajili ya shule za Msingi na Sekondari.

Hafla hiyo ya ugawaji wa vifaa hivyo ni mwendelezo wa shamrashara za kuadhimisha miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa Ruaha zilizoanza Oktoba Mosi, 2024 kwa kuzinduliwa na Machifu wa Mkoa wa Iringa waliotembelea hifadhi hiyo na kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana ndani ya eneo hilo.

Related Posts