Mwamayombo bingwa Hilali Cup, DC atoa neno uchaguzi

 

TIMU ya mpira wa miguu – Mwamayombo FC. kutoka kata ya Nyanguge imefanikiwa kutwaa ubingwa katika mashindano ya Hilali Cup 2024 baada ya kuichapa Bugohe Mlimani bao 1-0. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Fainali ya mashindano hayo yanayoandaliwa kila mwaka na Diwani ya Kata ya Nyangunge, Hilali Elisha, yamefanyika jana tarehe 6 Oktoba, 2024 mjini Nyagunge.

Washindi hao (Mwamayombo FC) walinyakua kombe pamoja na zawadi ya Sh 500,000 huku washindi wengine katika makundi mbalimbali wakipewa pia zawadi za pesa taslimu.

Akitoa zawadi kwa washindi wa mashindano hayo, Mkuu wa wilaya ya Magu, Joshua Nassari ambaye alikuwa mgeni rasmi katika fainali hiyo, alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kujiandikisha katika vitongoji vyao ili kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.

Alisema zoezi la kuandikisha wapiga kura katika uchaguzi huo litaanza tarehe 11 hadi 20 Oktoba mwaka huu huku kampeni zikitarajiwa kuanza tarehe 20 hadi 26 Novemba mwaka huu.

Naye Diwani wa Kata ya Nyanguge, Hilali Elisha mbali na kuwapongeza washindi wa mashindano hayo, pia aliwashukuru wananchi wa Kata ya Nyagunge kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo yaliyokuwa na mvuto wa kipekee.

About The Author

Related Posts