Sehundofe wakopeshana Sh bilioni 4.2 kujikwamua kiuchumi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Kikundi cha kuweka na kukopa cha Sehundofe kimetoa mikopo ya zaidi ya Sh bilioni 4.2 kwa wanachama wake kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Mikopo hiyo imetolewa tangu mwaka 2009 kikundi hicho kilipoanzishwa ambapo hadi sasa kina wanachama 758 wakiwemo wanawake 609 na wanaume 149.

Akizungumza Oktoba 5,2024 wakati wa maadhimisho ya miaka 15 ya kikundi hicho Katibu wa Sehundofe. Consolata Mangweha, amesema hadi sasa wamewekeza zaidi ya Sh bilioni 2.9 na wamefanikiwa kupata faida ya zaidi ya Sh milioni 213.3.

Amesema pia wamekuwa wakisaidiana pindi yanapotokea matatizo mbalimbali ambapo mwanachama akifariki kikundi hugharamia chakula, jeneza na usafiri na kusamehewa mkopo kisha kiasi alichowekeza hupewa watoto ili kukidhi mahitaji ya kielimu.

Kwa mujibu wa Mangweha, pia wameweza kutoa misaaada ya kijamii katika Shule ya Msingi Jeshini, Jica, Maghorofani, makanisa na misikitini.

Mkurugenzi wa Sehundofe ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalumu katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Semeni Mtoka, amesema kupitia kikundi hicho wanachama wengi wamenufaika kwa kuondokana na umaskini na kuwa kwenye kipato kinachoeleweka.

“Tuna vikundi 28 ambavyo vyote huwa vinakutana nyumbani kwangu, nimewajengea darasa. Tumefanikiwa kusomesha watoto, kujenga nyumba, kuna wenzetu wamenunua vitega uchumi kama bodaboda na wote tuna uhakika wa kipato,” amesema Mtoka.

Naye Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Ojambi Masaburi, amewataka wanachama wa kikundi hicho kuchangamkia mikopo inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Masaburi amesema halmashauri hiyo imetenga zaidi ya Sh bilioni 11.47 kwa ajili ya kukopesha makundi hayo na kwamba mikopo hiyo itaanza kutolewa hivi karibuni.

Katika hafla hiyo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema kikundi hicho ni mfano wa kuigwa kutokana na kuwaunganisha watu kutoka sehemu mbalimbali na kupeana mawazo ya kujikwamua kiuchumi.

Aidha amesema kupitia Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP 2) kilomita 72 zitajengwa kwa kiwango cha lami ikiwemo barabara ya Banana – Kitunda – Kivule – Msongola na ile ya Pugu – Majohe – Viwege – Njia nne na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu kusubiri mradi huo utekelezwe.

Jerry ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga, alikubali kuwa mlezi wa kikundi hicho na kuahidi kushirikiana na wanachama wa kikundi hicho kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Related Posts