Jeshi la Israel limetangaza hivi leo kuwa limetuma askari zaidi ili kuendeleza operesheni ya ardhini kusini mwa Lebanon. Kundi la Hezbollah limesema hii leo kuwa limewashambulia kwa kombora wanajeshi wa Israel katika mji wa mpakani wa Maroun al-Ras na kuwaua askari wawili wa Israel.
Makabiliano mengine yameripotiwa pia katika miji ya Udaissa na Kafr na maeneo mengine ya Lebanon . Mapigano yameripotiwa pia Gaza ambapo Mkuu wa shirika la misaada la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia Wapalestina UNRWA Philippe Lazzarini asema vita hivyo vilivyodumu kwa mwaka mmoja leo, vimeigeuza Gaza kuwa eneo la ‘makaburi’ na kusababisha mateso yasiolezeka.
Soma pia: Mwaka mmoja tangu shambulio la Hamas kusini mwa Israel
Hayo yanajiri wakati Israel ilikuwa inaadhimisha hivi leo kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kutokea kwa shambulio la Oktoba 7 ambapo wanamgambo wa Hamas walipovamia kusini mwa Israel na kuua watu takriban 1200 na kuwachukua mateka mamia ya wengine.
Tangu wakati huo, Israel inaendeleza mashambulizi makali dhidi ya kundi hilo huko Gaza na sasa imeanzisha vita vipya dhidi ya kundi la Hezbollah la huko nchini Lebanon.
Mshikamano na Israel na Miito ya kimataifa ya kutoutanua mzozo huo
Hata hivyo miito ya kimataifa imekuwa ikiendelea kutolewa na kuzitaka pande zote kujizuia ili kutolitumbukiza kwenye vita kamili eneo zima la Mashariki ya Kati.
Akiwa ziarani hivi leo mjini Tel-Aviv, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot amesema usalama wa Israel hauwezi kuhakikishwa kwa nguvu za kijeshi pekee bali kunahitahitajika pia suluhu ya kidiplomasia.
Naye, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema wanashikamana na Israel katika kumbukumbu ya mauaji hayo ya Oktoba 7 huku akitoa wito wa usitishwaji mapigano huko Mashariki ya Kati. Akitoa hotuba kwenye ufunguzi wa mkutano wa maendeleo endelevu katika mji wa kaskazini mwa Ujerumani wa Hamburg, Scholz amesema:
” Wapendwa marafiki zetu wa Israel, tuko pamoja nanyi katika hofu, uchungu, hali ya wasiwasi na huzuni. Tunasimama nanyi. Magaidi wa Hamas ni lazima wapigwe vita. Pia, ni wazi kwamba mwaka huu mmoja wa vita umesababisha mateso yasiyoweza kufikirika kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Matukio ya kila siku ya vurugu na njaa hayawezi kuwa msingi wa kuendeleza jambo jema. Watu wanahitaji matumaini na matarajio mema ili waweze kuachana na ugaidi.”
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema mwaka mmoja tangu shambulizi la Hamas, hali imezidi kuwa mbaya zaidi na Mashariki ya Kati imo ukingoni mwa vita kamili huku watu wa eneo hilo wakinaswa katika mzunguko usiokoma wa ghasia, chuki, na kulipizana visasi.
(Vyanzo: AP, DPAE, Reuters, AFP)