Waziri Mkuu atembelea mazoezi Stars

Na Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Oktoba 7,2024 ametembelea mazoezi ya timu ya Taifa, Taifa Stars inayojiandaa na michezo miwili ya kufuzu michuano ya AFCON 2025 dhidi ya DR Congo itakayochezwa Oktoba 10 na 15, 2024.

Taifa Stars inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wachezaji na benchi la ufundi katika mazoezi hayo, Majali amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassaan anamatumaini makubwa kuwa timu hiyo itafanya vizuri kwenye michezo yote miwili.

“Kila mmoja aone ana jukumu kubwa, kwako wewe mwenyewe na kwa nchi yako, Mheshimiwa Rais Dk. Samia anawatakia kila la kheri na alichofanya ametoa usafiri wa uhakika wa ndege itakayowapeleka nchini Congo kwa ajili ya mchezo wa Oktoba 10, 2024, hili ni jambo kubwa.”

Amewataka wachezaji hao kushikamana, kuzungumza lugha moja na kutanguliza uzalendo. “Tumieni fursa ya imani ya Watanzania kwenu kuiwakilisha vyema Tanzania kwenye michezo iliyo mbele yenu.”

Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo Mohammed Hussein “Tshabalala” amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kuwezesha kupatikana kwa usafiri wa ndege kwa ajili ya mchezo huo.

“Kwetu sisi hii ni motisha kuelekea michezo yetu miwili dhidi ya Congo, kwa sababu itatusaidia kurejea haraka nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa marudiano,” amesema Tshabalala.

Related Posts