WAZIRI NDEJEMBI ATOA MWEZI MMOJA KITUO CHA SEGESE KIANZE KUFANYA KAZI

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa mwezi mmoja Kituo cha Afya Segese kianze kufanya kazi mara moja baada ya kukamilika na kuwa na baadhi ya vifaa tangu mwaka 2023 hali inayosababisha wananchi waendelee kukosa huduma za afya ya uzazi na upasuaji.

Mhe Ndejembi ametoa maelekezo hayo  wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

“ Ninamuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya hapa Msalala kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa kituo hiki kinaanza kutoa huduma kwa wananchi. Lengo la Serikali ni kusogeza huduma karibu na wananchi na siyo kuwaacha watembee umbali mrefu. Hivyo ndani ya mwezi mmoja wananchi waanze kupata huduma hapa,” Amesema Mhe Ndejembi.

Aidha Waziri Ndejembi pia ameipongeza Kamati ya Shule ya Sekondari Ntobo iliyopo katika Halmashauri hiyo kwa kufanikiwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa gharama ya Sh Milioni 170.8 badala ya Sh Milioni 182 na hivyo kubakiza chenji ya Sh Milioni 11.1.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa shule hiyo, Mhe Ndejembi alisifu juhudi na uwajibikaji wa kamati ya ujenzi kwa kutumia fedha kwa ufanisi.

“ Kwa kawaida mara nyingi tunapokea taarifa za miradi ya maendeleo ambapo fedha huisha kabla ya mradi kukamilika lakini hapa Ntobo miradi imekamilika kwa kiwango cha juu na chenji imebaki. Haya ndio matumizi bora ya fedha za umma ambayo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anatuelekeza tuyafuate,” Amesema Mhe Ndejembi.

Katika ziara hiyo Waziri Ndejembi pamoja na kukagua miradi ya maendeleo pia alizungumza na wananchi wa Msalala ambapo aliwaeleza mafanikio makubwa yaliyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali ikiwemo za Afya, Elimu, Maji na Miundombinu katika Halmashauri hiyo.

Related Posts

en English sw Swahili