Israel imeongeza mashambulizi yake ya ardhini dhidi ya Hizbullah kando ya pwani ya kusini mwa Lebanon siku ya Jumanne, ikituma wanajeshi zaidi na kuwataka raia walio karibu na Bahari ya Mediterania waondoke.
Hizbullah inayoungwa mkono na Iran imesema imefyatua makombora kwenye mji wa Israeli wa Haifa, baada ya jeshi la Israeli kuripoti kwamba makombora 85 yalifyatuliwa kutoka Lebanon.
Ongezeko hili la sasa la mzozo huo linatokea baada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuapa kupigana “vita takatifu” hadi Hezbollah na Hamas washindwe.
Israel ilipanua operesheni zake nchini Lebanon takriban mwaka mmoja baada ya Hezbollah kuanzisha mashambulizi ili kuunga mkono mshirika wake wa Kipalestina, Hamas, kufuatia shambulio baya zaidi katika historia yake mnamo Oktoba 7, 2023.
Wakati ikipambana na Hamas huko Gaza, Israel imeapa kulinda mpaka wake wa kaskazini na Lebanon ili kuruhusu makumi ya maelfu ya Waisraeli waliokoseshwa makazi na mashambulizi ya kuvuka mpaka ya Hezbollah warudi nyumbani.
Hamas na Hizbullah zote zimeahidi kuendelea kupambana na Israel, na Jumanne naibu kiongozi wa Hezbollah Naim Qassem alisema kundi hilo litahakikisha Waisraeli hawawezi kurudi kaskazini, huku akisisitiza kuwa nguvu yao bado iko paleple.
”Nataka kuwahakikishia kuwa uwezo wetu ni mzuri na kile adui alichosema kuhusu uwezo wetu kuathiriwa ni njozi,” alisema Naim Qassem katika hotuba iliyorushwa kwa njia ya televisheni.
Yaunga mkono juhudi za kusitisha vita
Qassem alisema kuwa kundi hilo linaunga mkono juhudi za Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri – mshirika wa Hezbollah – kupata usitishaji vita, bila kutoa maelezo zaidi juu ya masharti yoyote kutoka kwa Hizbullah.
Soma pia: Netanyahu: Hakuna eneo tusiloweza kulilenga Mashariki ya Kati
Israel ilianzisha wimbi la mashambulizi dhidi ya ngome za Hezbollah Septemba 23, na kuwauwa watu wasiopungua 1,110 na kuwalazimisha zaidi ya milioni moja kukimbia.
Mashambulizi ya Israel yamelenga zaidi maeneo ya ngome za Hezbollah kusini na mashariki mwa Lebanon, pamoja na kusini mwa Beirut.
Wakati pwani ya kusini haikusazwa, onyo la hivi karibuni la Israel kuwata watu wahame linaashiria kwamba inapanua mashambulizi yake kuelekea kaskazini.
Kwenye kituo chake cha Telegram, jeshi la Israeli limesema Divisheni yake ya 146 ilianzisha oepresheni ndogo za ndani, na zenye malengo maalum dhidi ya shabaha na miundombinu ya Hizbullah kusini magharibi mwa Lebanon.
Israel yasema huenda mrithi wa Nasrallah aliuawa pia
Katika kile ambacho kinaweza kuwa pigo la karibuni zaidi katika mfululizo wa mapigo makubwa kwa Hizbullah, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema inaonekana mrithi wa kiongozi wa Hizbullah aliyeuawa Sayyed Hassan Nasrallah naye pia ameshauawa.
Soma pia: Naibu Mkuu wa Hezbollah: Tuko tayari kwa lolote
Hashem Safieddine, afisa wa juu wa Hizbullah alitarajiwa na wengi kumrithi Nasrallah, lakini hajasikika hadharani tangu shambulizi la Israel mwishoni mwa wiki iliyopita.
Gallant amewaambia maafisa katika kamandi ya kaskazini ya jeshi la Israel kupitia ujumbe mfupi wa vidio, kwamba Hizbullah ni kundi lisilo la kiongozi, na kwamba hakuna wa kufanya maamuzi wala kuchukuwa hatua.
Hata hivyo, Naim Qassem amesema katika hotuba yake kuwa kundi hilo limeweza kuziba nafasi zote za makanda wake waliouawa, na kwamba uchaguzi wa katibu mkuu unatatizwa tu na mashambulizi ya mfululizo ya Israel.