SERIKALI YATOA MAAGIZO TISA KWA WAKUU WA TAASISI ZA UMMA

Kibaha, Pwani, Oktoba 7, 2024. Serikali imetoa maagizo tisa kwa watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali kwa lengo la kuongeza ufanisi katika maeneo yao husika ya kazi na hatimaye kuongeza mchango wao kwa Taifa.

Maagizo hayo yalitolewa Wilayani Kibaha, mkoani Pwani Jumatatu (Oktoba 7, 2024) na Dkt. Tausi Kida, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt Moses Kusiluka, wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa watendaji wakuu wapya 111 wa taasisi za umma.

Maagizo hayo yaliyotolewa, ni pamoja na kufanya usimamizi madhubuti wa taasisi ili kuwezesha utekelezaji mzuri wa majukumu, kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya serikali na kuendelea kujifunza ili kujenga uwezo wa taasisi za umma.

Maagizo mengine ni usimamizi madhubuti wa rasilimaliwatu, rasilimali fedha pamoja na rasilimali nyingine za serikali zilizowekezwa katika taasisi, na kujenga uhusiano wa kiutendaji wenye afya baina yao na watumishi wanaowasimamia, bodi za wakurugenzi, wizara mama pamoja na wadau wengine.

Pia, Dkt. Kida aliwataka watendaji wakuu wa taasisi za umma kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato, kuimarisha matumizi ya TEHEMA, kuimarisha mifumo ya utoaji huduma, na kujenga maadili mema mahala pa kazi ili kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Programu ya mafunzo hayo ya siku tatu imeandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Taasisi ya Uongozi kwa lengo la kuwajengea uwezo watendaji wakuu wapya ili watekeleze majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Akifungua mafunzo hayo, kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Kida aliwakumbusha watendaji hao kuwa taasisi na mashirika wanayoyaongoza ni mali ya umma, hivyo umma unatarajia kuona matokeo chanya na yenye maslahi kwao.

“Lazima tuweke mbele maslahi mapana ya Taifa katika kuziongoza taasisi ili nchi ifaidike na uwepo wa taasisi hizi,” alisisitiza.

Dkt. Kida alisema program ya mafunzo kwa watendaji walioteuliwa ni kielelezo dhahiri cha dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha kuwa watendaji wanajua nini wanatakiwa kwenda kufanya katika taasisi walizopewa kuongoza.

Alimpongeza Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu pamoja na timu yake kwa mageuzi yanayoendelea katika utendaji kazi wa taasisi za umma.

“Mageuzi haya kwenye taasisi na mashirika ya umma ni kielelezo tosha cha uongozi imara chini ya Ofisi yako. Natoa wito kuendeleza jitihada hizo ili tuongeze ufanisi,” alihitimisha Dkt. Kida.

Kwa upande wake Bw. Mchechu, alisema kama watendaji wakuu wakitekeleza kwa umadhubuti ujuzi na mbinu mbalimbali watakazopata katika mafunzo, wataweza kusimamia taasisi zao na kuziendesha kwa ufanisi na hatimaye kufanikisha malengo yaliyowekwa na serikali.

“Lengo la mafunzo haya ni kuongeza tija na ufanisi katika taasisi mnazozisimamia,” Bw Mchechu aliwaambia watendaji wakuu wa taasisi za umma.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanayohusisha watendaji wakuu walioteuliwa kuanzia mwaka 2022 mpaka 2024, yatakuwa endelevu, kwa mujibu wa Bw. Mchechu, na kwamba yatakuwa yanafanyika kila baada ya miezi sita.

Aliongeza kuwa programu hiyo ya mafunzo ni mwendelezo wa hatua mbalimbali ambazo Ofisi ya Msajili wa Hazina inachukua katika kutafsiri na kutekeleza kwa vitendo maono ya Mheshimwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na falsafa ya 4Rs.

“Katika falsafa ya 4Rs tumejikita katika R mbili kati ya nne ambazo ni Reform na Rebuild,” alisema.

Alifafanua: ”Hapa tutajikita zaidi katika eneo la kuwajengea uwezo watendaji wakuu ili wawe na ufanisi zaidi katika usimamizi wa taasisi za umma.”

Katika nchi hii kuna taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali 309 ambapo uwekezaji wake ni Sh75.8 tirioni, kwa mujibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida akifungua mafunzo elekezi kwa watendaji wakuu wapya 111 wa taasisi za umma kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt Moses Kusiluka, hafla ambayo imefanyika Oktoba 7,2024 Kibaha mkoani Pwani.

Related Posts