Spika wa baraza la seneti Amason Kingi nchini ametangaza kuwa mapema hii leo amepokea taarifa ya hoja iliyopitishwa na bunge jana likiunga mkono kutokuwa na Imani na naibu wa rais Rigathi Gachagua baada ya wabunge 282 kuipigia kura ya ndio hoja ya kumuondowa Gachagua.
Baraza hilo limeanza na hatua ya kujadili namna vikao vya kusikiliza hoja hiyo vitafanyika ambapo maseneta wengi wamesisitiza iwasilishwe na kujadiliwa kwenye baraza la seneti ili kumpa kila mmoja fursa ya kutoa maoni yake, kinyume na pendekezo alilotoa Kiongozi wa wengi kwenye seneti Aaron Cheruyiot la kuundwa kwa kikao maalum cha maseneta 11 kuisikiliza hoja yenyewe kabla haijawasilishwa kwenye baraza zima kupigiwa kura. Spika wa bunge la Seneti Amason Kingi ameeleza kuwa
“Pendekezo la kamati maalum limekataliwa. Hivyo baraza la seneti litaendelea na uchunguzi wa hoja ya kumuondoa madarakani naibu wa rais Rigathi Gachagua katika kikao kizima cha baraza.”, alisema Kingi.
Maoni mseto ya Wakenya
Huku wakiendelea kutoa maoni yao kuhusu kuondolewa madarakani, Wakenya wamegawanyika huku baadhi wakiiomba serikali kuhakikisha mchakato huo hauongezi joto la kisiasa nchini humo.
Baadhi ya wabunge wanaomuunga mkono naibu wa rais wameeleza kusikitishwa kwao na bunge kutozingatia maoni ya umma yaliyorekodiwa katika mchakato wa ushiriki wa umma uliofanyika wiki iliyopita kuambatana na hoja ya kumuondoa madarakani Naibu wa Rais Rigathi Gachagua.
Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba anasema kwa kutozingatia maoni ya Wakenya, kunaonyesha kwamba mchakato huo hauna umuhimu.
“Nimekata tamaa sana kwa sababu Wakenya walijitokeza kwa wingi wakati wa ushiriki wa umma, na walijaza nakala hizo nyingi sana na kusema walichotaka, lakini spika amepuuza kabisa hilo”, alisema Wamuchomba.
Macho yote sasa yameelekezwa kwenye baraza la seneti ambapo spika Kingi ameahidi kwamba bunge la seneti litatenda haki kuitazama hoja hiyo na hakutakuwa na malalamiko yoyote.