Bunge la Kenya lapiga kura ya kumuondoa madarakani Gachagua – DW – 09.10.2024

Naibu wa rais Rigathi Gachagua sasa anasubiri kuijua hatma yake wakati baraza la Senate litakapojadili hoja hiyo na kuipigia kura.

Kiongozi huyo alikabiliwa na makosa 11 ya ufisadi, kutumia vibaya madaraka na kukiuka katiba. Hii ni mara ya kwanza kwa naibu wa rais kuondolewa madarakani kwa njia hii chini ya katiba mpya ya 2010. 

Cheche zilitawala bungeni wakati wa mjadala wa kumtimua naibu wa rais Rigathi Gachagua. 

Baada ya zaidi ya saa saba za majadiliano, wabunge 281 walipiga kura kuridhia kumtimua naibu wa rais huku 44 wakipinga na mmoja akisusia.

Soma pia:  Wakenya washiriki mdahalo wa kumuondoa makamu wa rais

Mishi Mboko ambaye ni mbunge wa Likoni amemnyoshea kidole cha lawama Gachagua kwa kuchochea ukabila.

Sasa hatua inayofuata ni Spika wa Bunge la taifa Moses Wetangula kuwasilisha ujumbe kwa mwenzake wa baraza la Senate Amason Kingi katika kipindi cha siku mbili kama inavyoagiza ibara ya 145 sehemu ya pili A ya katiba.

Gachagua kujitetea mbele ya bunge la Seneti

Kenya | Bunge
Bunge la KenyaPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Kwa upande wake, spika wa baraza la Senate atalazimika kuita mkutano ndani ya muda wa wiki moja ili kuyatathmini makosa anayotuhumiwa naibu wa rais.

Kimsingi ibara hiyo hiyo ya 145 katika sehemu ya tatu B inailazimu Senate kuunda kamati maalum ya wanachama 11 kuchunguza tuhuma katika kipindi hicho na kuandaa ripoti. Endapo thuluthi mbili ya maseneta wote 67 watapiga kura kuunga mkono kila shtaka lililofikishwa mbele yao, Rigathi Gachagua atatimuliwa. Maseneta wasiopungua 45 ndio wanaoweza kulitimiza hilo.

Soma pia: Gachagua akanusha madai ya ufisadi na kujilimbikizia mali

Hoja ya kumwondoa Gachagua madarakani iliwasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse. Itakumbukwa kuwa wabunge walianzisha mchakato wa kumtimua Gachagua Oktoba mosi mwezi huu pale 291 walipotia saini hoja ya kumtimua.

ZamZam Mohamed ambaye ni mbunge wa kaunti ya Mombasa amesema naibu wa rais ana matatizo.

Wakati huo huo, sauti ya umma ilipata sikio na maoni kukusanywa na kuwasilishwa bungeni mwanzoni mwa wiki hii. Kulingana na ripoti ya matokeo, asilimia 65.1 waliunga mkono hoja ya kumtimua.

Ifahamike kuwa mwaka 1989 makamu wa rais wa wakati huo Dkt Josephat Karanja alijiuzulu alipojikuta kwenye hali kama hii ya wabunge kutaka kumtimua.

 

Related Posts