ELISHA MNYAWI MWENYEKITI MPYA MAREMA

Na Mwandishi wetu, Babati

MCHIMBAJI maarufu wa madini ya Tanzanite na madini ya viwandani Elisha Nelson Mnyawi amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA).

Afisa madini mkazi (RMO) wa Manyara, mhandisi Godfrey Nyanda akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika mjini Babati, amesema Elisha ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura 61 kati ya kura 101.

RMO Nyanda amesema Elisha amepata nafasi hiyo kwa kumshinda mgombea mwenzake Joseph Manga aliyepata kura 38 huku kura mbili zikiharibika.

Amesema Money Yusuf ametetea nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti MAREMA kwa kupata kura zote 101 huku Tariq Kibwe akifanikiwa kutetea tena nafasi ya Katibu kwa kura zote 106.

Amesema mgombea wa nafasi ya Katibu msaidizi Dkt Curtius Msosa ambaye hakuwa na mpinzani kwenye mchuano huo amechaguliwa kwa kupata kura 96.

“Aliyekuwa Mweka hazina wa MAREMA, Neney John Lyimo amefanikiwa kutetea nafasi hiyo kwa kupata kura 70 huku Fatuma Msangi akipata kura 31,” amesema RMO mhandisi Nyanda.

Amesema mgombea Samuel Rugemalira amefanikiwa kuchaguliwa kuwa Mweka hazina msaidizi baada ya kupata kura zote 101za ndiyo.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo Mwenyekiti mpya wa MAREMA Elisha Nelson Mnyawi amewaahidi ushirikiano wa kutosha na kuwaunganisha wachimbaji wote.

“Nimetembelea matawi mbalimbali na kufika hadi Magara na Magugu ila sijaridhishwa na ofisi yao hivyo nawaagiza viongozi wa Tawi hilo watafute ofisi nyingine nitalipia pango kwa mwaka mmoja na baadhi ya samani za ofisi nitanunua,” amesema Elisha.

Katibu Tawala (DAS) wa Wilaya ya Babati, Khalifan Matipula ameupongeza uongozi ulipita wa MAREMA kwa kumaliza kipindi chao kwani walitekeleza vyema majukumu yao na anatarajia viongozi wapya wataendeleza mazuri yaliyofanyika.

Mwenyekiti mstaafu wa MAREMA Justin Nyari amempongeza Elisha kwa kupata nafasi hiyo ya kuwatumikia wachimbaji wa madini wa mkoa wa Manyara.

Related Posts