Akizungumza kutoka ikulu ya Marekani ya White House hapo jana, Rais Biden alisema kimbunga Milton ni suala la hatari kwa usalama na kuwahimiza wale waliopewa maagizo ya kuhama kufanya hivyo mara moja.
Wakazi wa Florida wachukuwa tahadhari dhidi ya kimbunga Milton
Katika tukio la maandalizi lililoonekana kufanyika kote jimboni Florida, magari kadhaa yalijipanga kwenye kituo kimoja cha michezo huko Tampa ili kubeba magunia ya mchanga kuzilinda nyumba zao dhidi ya mafuriko huku wengine wakikimbia eneo hilo.
Safari za ndege zaongezwa katika maeneo yanayokabiliwa na hatari
Mashirika ya ndege yaliongeza safari za ndege kutoka Tampa, Orlando, Fort Myers na Sarasota, huku barabara kuu zikiwa na misongamano ya magari yaliokuwa yakitoka eneo hilo na vituo vya kuuza petroli vikiripotiwa kuishiwa na bidhaa hiyo muhimu.
Soma pia:Kimbunga Milton chaongezeka kasi kuelekea Mexico
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa Kituo cha utabiri wa matukio ya vimbunga nchini Marekani (NHC) Michael Brennan, kufikia jana, kimbunga hicho kilikuwa kimefikia ngazi ya tano ya ukubwa katika kipimo kinachotumiwa kupanga kitisho cha vimbunga.
Katika mkutano na waandishi habari, gavana wa Florida Ron DeSantis, alitaja miji inayokabiliwa na hatari ya kimbunga hicho na kusema kimsingi eneo zima la rasi ya Florida liko chini ya aina moja ama nyingine ya tahadhari.
Mtaalamu wa vimbunga Michael Lowry, ameonya kuwa katika eneo la Tampa ambalo ni makazi kwa takriban watu milioni 3, huenda kimbunga Milton kikasababisha athari maradufu ya zile zilizoshuhudiwa wiki mbili zilizopita wakati kimbunga Helen kilipopiga na kusababisha mafuriko makubwa.
Donald Trump ashtumu juhudi za serikali za kukabiliana na dharura
Baada ya kimbunga Hellen, rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alitumia changamoto za juhudi za kukabiliana na hali za dharura pamoja na taarifa potofu, kudai kwamba pesa za kushughulikia majanga badala yake zimetumika kuwashughulikia wahamiaji.
Rais Biden akosoa matamshi ya Trump
Kwa upande wake hapo jana Rais Biden aliyashtumu matamshi ya Trump na kuyataja kutokuwa ya kizalendo, huku naibu rais Kamala Harris akionya kuhusu athari za habari potofu dhidi ya juhudi za serikali.
Rais Biden aahirisha ziara za Ujerumani na Angola
Rais Biden ameahirisha ziara kubwa nchini Ujerumani na Angola kusimamia juhudi za kukabiliana na hali hiyo ya dharura huku juhudi za kutoa misaada wakati wadhoruba zikiibuka kama suala la kisiasa kabla ya uchaguzi wa rais mnamo Novemba 5.