LSF, kwa kushirikiana na wadau wake NORTH-SOUTH COOPERATION kutoka Luxembourg, imekamilisha mradi wa miaka miwili unaojulikana kama ‘Wanawake Tunaweza,’ ambao umeleta mafanikio makubwa katika kuwawezesha wanawake na watoto wa kike kutoka jamii ya Kimasai wilayani Longido.
Mradi huu, ulioanza kutekelezwa mwaka 2022, umelenga kuwawezesha wanawake na wasichana kijamii na kiuchumi kwa kuwajengea uwezo kupitia vikundi vya wanawake 11 na kuwaanzishia miradi mbalimbali ya ujasiriamali kama vile ufugaji wa mifugo, uuzaji wa nafaka, utengenezaji wa urembo wa Kimasai, kilimo cha bustani, pamoja na shughuli za VICOBA.
Kupitia mradi huu, akinamama wameweza kuanzisha kikundi cha pamoja kijulikanacho kama ‘Osiligi’ na wamepatiwa vyerehani 11 kwa ajili ya kushona taulo za kike zinazotumika tena (Reusable Sanitary Pads). Taulo hizi zimesaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa kike katika shule za Lekule na Namanga, ambao ni miongoni mwa wanufaika wakuu.
Mbali na hayo, mradi umeweza kuwasaidia watoto wa kike kupata mazingira bora ya kusomea kwa kujenga mabweni mapya, huku zaidi ya wasichana 1,214 wakiwa wamefaidika kupitia shughuli mbalimbali za elimu, usawa wa kijinsia, na haki zao za msingi.
Aidha, zaidi ya wanawake 209 wamenufaika moja kwa moja katika eneo la ujasiriamali, huku jumla ya watu 2,500 wakiwemo wanaume na wanawake wa Longido wakielimishwa juu ya masuala ya kijinsia na haki ya mwanamke kwa kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huu.
Mradi pia umeweza kuwajengea uwezo viongozi wa kimila takribani 20, huku wakishirikiana na wanaume shupavu (Male Champions) 7 waliopatiwa mafunzo maalum kupitia shirika la WASHEWILO, ambalo pia linapata ufadhili kutoka LSF, ili kuleta mabadiliko chanya katika mtazamo wa jamii kuhusu haki za wanawake.
Mafanikio mengine makubwa ni kuboresha chumba cha Tehama (ICT room) katika shule ya Namanga, kwa kuweka kompyuta, viti, na vifaa vya kisasa vinavyowezesha wanafunzi 40 kupata elimu ya Tehama kwa wakati mmoja.
Pamoja na maboresho haya, kampeni ya upandaji miti katika mashule na jamii imewezesha miche 1,420 kupandwa na kuhudumiwa licha ya changamoto ya ukame kwenye eneo hilo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mradi huu, Meneja Mawasiliano wa LSF alitoa wito kwa serikali ya wilaya na wadau wengine kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanadumishwa na kuendelezwa.
Alisisitiza kuwa, licha ya hatua kubwa iliyofikiwa, bado kuna maeneo ya kuboresha hasa katika kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa na wanawake wa vikundi hivyo na kuhakikisha kuwa mipango ya kuwasaidia kinamama hao inafuatiliwa na kutekelezwa kikamilifu.