MAGRETH BARAKA AJITOSA UENYEKITI VIJANA FEMATA

Na Mwandishi wetu

MKURUGENZI wa kampuni ya Mfuko wa Uwekezaji wa Madini wa Afrika (Africa Investment Fund) Magreth Baraka Ezekiel ametia nia ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa vija Taifa wa shirikisho la vyama vya wachimbaji madini nchini (FEMATA).

Magreth ambaye ni Mkurugenzi wa mfuko huo wa AIF unaowaunganisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika kuwekeza kwenye migodi barani Afrika ni binti wa mchimbaji maarufu wa madini ya dhahabu Baraka Ezekiel mwana maono ambaye historia inamtambua kwa kuanzisha wazo la wachimbaji madini kuwa na benki yao.

Magreth amesema yeye akiwa binti wa mchimbaji mzawa anajivunia sana kuwa sehemu ya sekta muhimu ya madini aliyoifahamu tangu utoto wake.

“Uchimbaji wa madini ni maisha yetu, urithi wetu kutoka kwa Taifa letu na viongozi wetu, wakiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mtetezi mkubwa wa sekta hii, mimi kama binti nasimama pia kuunga mkono juhudi za mama katika kuitetea sekta hii na kuiletea mafanikio makubwa,” amesema Magreth.

“Nina amini kwamba umoja wetu ndiyo nguvu yetu, madini yetu ni urithi wetu na vjana wetu ni dhahabu yetu, kama kijana niliyezaliwa na kulelewa kwenye sekta hii naomba kwa unyenyekevu mkubwa fursa ya kuwania kuwa Mwenyekiti wa vijana Taifa kupitia FEMATA,” amesema Magreth.

Amesema ana amini katika maono yake ya kuunga mkono dira ya Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde kupitia mpango wa Madini 2030 na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kuongeza uwekezaji katika sekta ya madini.

Amesema vijana ni jeshi kubwa na jukumu lao ni kuibeba sekta na kuja na mawazo mapya na chanya kwa ajili ya kuiendeleza sekta ya madini.

“Kwa maneno ya baba yangu mtoto mwema ni yule anayekuta kuna milioni 10 na yeye anatafuta milioni 100 na kuongeza uchumi wa familia, naomba mnipe fursa ya kuinuka pamoja na vijana wenzangu na familia nzima ya FEMATA,” amesema Magreth.

Ameahidi baadhi ya vitu atakavyofanya pindi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Vijana Taifa kupitia FEMATA ni kuunganisha vijana waliopo kwenye uuzaji, uchakataji na mnyororo mzima wa thamani ya madini, ikiwemo vijana wanaoongeza thamani kwenye madini ya vito, dhahabu na madini ya kimkakati, wanaosomea jiolojia, wauza kemikali na vifaa vya uchimbaji ambavyo watatumia mablasta, fundi matimba na waponchaji na kila kijana anayeshiriki kwa namna moja au nyingine katika sekta.

“Kuongeza na kushawishi uwekezaji kwenye migodi kwa kutumia wawekezaji wa ndani na nje kwa ajili ya kuongeza teknolojia katika kitovu cha uchimbaji ambao ni utafiti wa madini,” amesema Magreth.

Amesema vijana kuwezeshwa na kupatiwa leseni na mtaji kupitia mfuko wa uwekezaji wa madini wa vijana utakaoanzishwa kwa ajili ya kuwa na miradi endelevu inayowainua vijana kiuchumi na kuleta muendelezo wa uchimbaji.

“Benki ya wachimbaji, nitahamasisha uanzishaji wa Benki ya wachimbaji itakayowezesha wachimbaji vijana kupata mikopo kwa masharti nafuu ili waweze kujiajiri na kuimarisha shughuli zao kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha, wawekezaji na wadau mbalimbali,” amesema Magreth.

Amesema mfuko wa uwekezaji madini wa vijana, shirikisho lina vijana takribani milioni 3 kila kijana akichangia shilingi elfu 10 mfuko wa vijana utakuwa na takribani bilioni 3 ya awali kuwekeza kwenye sekta mbalimbali kama vile elimu, vifaa na teknolojia, uwezeshwaji wa ajira ambao kila kijana kwa mwaka 2030 kupitia mfuko atakuwa na uwezo wa kupata zaidi ya milioni 200 ikiwa Uwekezaji kwenye mradi utakuwa endelevu.

“Kila kijana kumiliki leseni ya uchimbaji pamoja na asilimia ya kudumu ili kufanya uchimbaji kuwa biashara endelevu, Bina ya Afya kwani vijana wengi wanavyopata majanga wanashindwa kumudu gharama hivyo bima itawasaidia kwa asilimia 98 ya matibabu, hii itasaidia kupunguza hatari zinazohusiana na kazi ya uchimbaji na kuhakikisha ustawi wa familia zao,” amesema Magreth.

Amesema pia kuongeza wigo kwa mabinti kwenye uchimbaji, uwekezaji na mnyororo mzima wa madini, kujenga uongozi imara wa vijana na kuwekeza katika elimu ya madini.

“Umoja wetu, nguvu yetu, madini yetu ni urithi wetu na vjana ni dhahabu yetu, kwa unyenyekevu wa hali ya juu na matumaini makubwa juu ya mabadiliko katika sekta yetu ya madini naomba kura yako ya kipekee, nikiwa tayari kutumikia Taifa langu, wachimbaji wenzangu na kwa vijana wenzangu katika kuinua sekta yetu, uchumi wetu na Taifa kiujumla Mungu awabariki, Madini ni maisha na utajiri,” amesema Magreth.


Related Posts