Wafanyakazi wengi wa kujitolea wamekimbia kutokana na kitisho cha kukamatwa ama vurugu, na majiko kadhaa ya jumuiya ambayo yalikuwa yameanzishwa katika taifa hilo ambako mamia ya watu wanakadiriwa kufa kwa njaa na magonjwa yanayohusiana na njaa, wameacha kutoa huduma muhimu ya milo ya kila wiki.
Shirika la habari la Reuters lilizungumza na wafanyakazi 24 wa kujitolea wanaosimamia majiko ya jumuiya katika jimbo la kati mwa Sudan la Khartoum, eneo la magharibi la Darfur na sehemu za mashariki ambako mamilioni ya watu wamekimbia makaazi yao tangu kuzuka kwa mapigano kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF.
Mashirika ya Kimataifa ya kibinadamu ambayo yameshindwa kufikisha msaada wa chakula katika maeneo yaliyo kwenye hatari ya kutumbukia katika njaa, yameongeza juhudi zaidi za kupeleka msaada katika maeneo hayo. Hata hivyo zoezi hilo limekuwa likilengwa na mashambulizi ya wanamgambo wa RSF.
Soma pia:Marekani yaridhishwa na usambazaji misaada Sudan
Wafanyakazi kumi wa kujitolea walisema: “walikuwa salama wakati RSF haikujua kuhusu ufadhili,”: alisema Gihad Salaheldin, mfanyakazi wa kujitolea ambaye alikimbia mjini Khartoum mwaka jana.
Baadhi ya wafanyakazi wa kujitolea ambao walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina kwa hofu ya kulipiziwa kisasi wameongeza kwamba pande zote mbili za mzozo zinawashambulia au kuwaweka kizuizini wafanyakazi wa kujitolea kwa tuhuma za kushirikiana na upande hasimu.
Visa vya mashambulizi vyahusisha pande zote za mzozo
Mmoja wa wafanyakazi wa kujitolea katika mji wa Bahri, alisema wanajeshi waliovalia sare za RSF waliiba simu walizotumia kupokea michango pamoja na pauni milioni 3 za Sudan fedha taslimi zilizokusudiwa kwa manunuzi ya chakula mwezi Juni.
Kisa hicho kilichoathiri mamia ya watu waliokuwa wakitegemea msaada katika jiko hilo la jumuiya kilikuwa moja ya matukio matano katika mwaka huu, ambapo mfanyakazi huyo wa kujitolea alishambuliwa na wanamgambo wa RSF wanaodhibiti vitongoji kadhaa vilivyo na majiko yapatayo 21 yakihudumia watu takriban 10,000.
Katika tukio kama hilo askari ambao hawakuainishwa ni wa upande gani wa mzozo walivamia moja ya nyumba ya jiko la jumuiya usiku wa manane na kuiba magunia kadhaa ya uwele na maharage.
Soma pia:Sudan yapinga kuushambulia ubalozi wa UAE
Mhudumu wa kujitolea ambaye alikuwa amelala hapo, alisema alifungwa, kuzibwa mdomo na kuchapwa viboko kwa saa kadhaa na wanajeshi waliotaka kujua ni nani anayefadhili harakati hizo.
Majiko mengi nchini Sudan, hayahifadhi taarifa juu ya mashambulizi huku wengine wakihofia kuzungumza kwa usalama wao.
Hata hivyo wafanyakazi wa kujitolea walielezea visa takriban 25 ambavyo vinalenga moja kwa moja majiko ya jumuiya au wafanyakazi wake wa kujitolea kwa mwezi wa Julai pekee.
Mashirika ya kiutu yanayoendesha majiko hayo yametangaza vifo vya wafanyakazi wa kujitolea wasiopungua watatu katika mashambulizi ya moja kwa moja ikiwemo kupigwa risasi na kuuwana na wanamgambo wa RSF mnamo mwezi Septemba.
Wadau: Kundi hili halipewi thamani
Mkuu wa Baraza la wakimbizi la Norway nchini Sudan, Mathlde Vu, anasema pande zote zinazohasimiana Sudan zimeshindwa kutambua umuhimu wa kundi hilo kwenye mfumo wa usalama wa raia hasa wanaokabiliwa na mzozo wa chakula katikati ya mapigano.
“Haya yote ni sehemu ya pande zinazohasimiana kutoheshimu ulinzi wa raia.”
Alisema Mathlde na kuongeza kwamba wafanyakazi hao ni muhimu kwenye mfumo wa kibinadamu, na chini ya sheria ya kimataifa za kiutu wanapaswa kulindwa, lakini kwa bahati mbaya hawako salama kabisa.
Soma pia:RSF: Tuko tayari kutekeleza mpango wa usitishwaji mapigano
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema zaidi ya nusu ya wakazi wa Sudan sawa na watu milioni 25.6, wanakabiliwa na njaa kali na wanahitaji msaada wa haraka.
Tumaini walilokuwa nalo ni majiko hayo ya jumuiya nalo sasa liko mashakani kutokana na usalama duni wa wafanyakazi wake wa kujitolea.