Katika mahojiano maalumu na Idhaa ya Kiingereza ya DW, kwenye mkutano kuhusu nishati endelevu uliofanyika Oktoba 7 mjini Hamburg, nchini Ujerumani, rais Mbumba amesema ukame umesababisha athari kubwa nchini Namibia kwa kuwa hakuna nafaka na chakula. Ardhi imekauka sana na ameziagiza afisi za waziri mkuu, naibu waziri mkuu, waziri wa usafiri, waziri wa kilimo na waziri wa maji zihakikishe malori yanaendelea kusambaza maji kuwapelekea raia wenye mahitaji.
“Kumekauka sana, lakini tuna matumaini mvua zitaanza kunyesha hivi karibuni na watu wataanza kupanda tena mazao yao kama vile mtama, uwele, mahindi na maisha yao yatarejea katika hali ya kawaida.”
Ukame umezikumba pia nchi nyingine wanachama wa jumuiya ya kiuchumi ya kusini mwa Afrika, SADC. Rais Mbumba alisema ushirikiano upo kati ya nchi za jumuiya hiyo, huku Tanzania ikiwa nchi pekee ya SADC iliyozalisha mahindi mengi ya kutosha kwa hiyo watayanunua.
Alisema Zimbabwe ni nchi ambayo inatarajia mavuno mazuri ya ngano kwa hiyo watafanya biashara ya kununuliana na kuuziana bidhaa. Hata hivyo amesema wanatarajia msaada kutoka nchi nyingine kwa sababu kiujumla wanakabiliwa na ukame na haingii akilini kuficha ukweli kuhusu janga kubwa kiasi hiki.
Suala la fidia
Kuhusu fidia kwa mateso yaliyofanya wakati wa ukoloni wa Ujerumani nchini Namibia, rais Mbumba alisema suala la mauaji ya kiholela linatakiwa kushughulikiwa katika ngazi tofauti na taasisi itakayoundwa kurekebisha kilichoharibiwa na kujaribu kurejesha kilichopotea itakuwa na mamlaka yake kuweza kufanya hivyo; kwa hiyo haitakiwi kuwa fidia itakayosaidia kujenga shule.
Rais Mbumba amesema haiwezekani kila mtu katika jamii ya Namibia kuja Ujerumani kufanya mashauriano na haiwezekani pia kwa kila Mjerumani kuja kwenda Namibia kufanya majadiliano. Ni muhimu kujadiliana katika mamlaka ya ngazi ya dola. Kwa hiyo wamekuwa wakizungumza na viongozi wao wa jadi, lakini katika kila jamii kuna demokrasia na kuna maoni tofauti tofauti. Hii hata hiyo haina maana kwamba hawajawashirikisha raia wa Namibia katika suala zima la kudai fidia kutoka kwa Ujerumani.
Mradi wa nishati ya hydrojeni
Njia moja ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa imekuwa kuanzisha miradi ya nishati inayotokana na gesi ya hydrojeni, kama ule unaoendeshwa nchini Namibia pamoja na Ujerumani.
Alipoulizwa kuhusu nishati safi ya gesi ya hydrojeni, rais Mbumba alisema wamejitolea kwa dhati kwa mradi huo na kwa mara ya kwanza wahandisi na wachora ramani za majengo na mafundi wanakuja katika vyuo vikuu vya Ujerumani kujifunza jinsi ya kuendesha viwanda hivyo.
“Na tunajivunia hilo. Tuko mbele ya nchi nyingine za bara la Afrika. Tunafanya kazi pamoja na Afrika Kusini. Tunafanya kazi pamoja na nchi nyingine za kiafrika na nyingine duniani zinazotaka kushirikiana na sisi. Sio Ujerumani tu ambayo imejihusisha kushirikiana na sisi katika suala la nishati safi inayotokana na gesi ya hydrojeni.”
Suala la msamaha
Ujerumani imetajwa kuwa miongoni mwa nchi washirika katika mradi wa hydrojeni lakini bado kuna mtihani kuhusu madai ya fidia ya mauaji ya halaiki yaliyofanywa enzi ya ukoloni wa Ujerumani nchini Namibia. Rais Mbumba alihoji mtu anapofanya kosa na anapolitambua anatakiwa kuchukua hatua na anyoshe mkono kwa mtu aliyemkosea.
“Kama ni mtu mwenye nguvu na ari njema, unaomba msamaha. Na utaandaa mazingira ya kufuta makosa yaliyofanywa. Na hilo ndilo ambalo tumekuwa tukijadiliana. Kuhusu suala la mauaji ya halaiki,ilichukua muda lakini Nambia na Ujerumani zimekubaliana yalifanyika. Halafu suala la msamaha hawajatilia shaka, wamesema wako tayari kuomba msamaha.”
Soma pia: Serikali ya Ujerumani kutekeleza yaliyofikiwa kati yake na Namibia
Kiongozi wa Namibia anasema suala nyeti ni jinsi ya kulipa fidia kwa maisha yaliyopotea, sio tu katika vita bali pia katika kambi za mateso. Suala la kupora ardhi na ng’ombe wao wote na mali zao nyingine. Rais Mbumba anakiri pamekuwa na changamoto katika kupima thamani ya gharama ya vitu vilivyopotea na kile kinachoweza kufanywa sasa.
Hata hivo rais huyo wa Namibia ana matumaini kwa nia njema patapatikana njia kuonesha kwamba kosa lililofanywa limetambuliwa na kulipiwa fidia. Amesema ni mchakato unaotakiwa kufanyika hatua kwa hatua ili jamii ijihisi imelipwa fidia na kufutwa machozi katika madai yao ya fidia.