Watengenezaji mkaa mbadala waitwa Tirdo kuongeza ujuzi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limesema watengenezaji wengi wa mkaa mbadala bado wanatumia mabaki ya mkaa unaotokana na kuni na kuwahamasisha kwenda kupata mafunzo kwa kuwa wametengeneza kanuni mbalimbali za ujifunzaji.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Profesa Mkumbukwa Mtambo, akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi wa Kukuza Matumizi ya Mkaa Mbadala, Dar es Salaam.

Kulingana na shirika hilo, zaidi ya asilimia 50 ya sampuli 43 za mkaa mbadala zilizopimwa zilibainika kutokuwa na ubora.

Akizungumza Oktoba 7,2024 kuhusu utekelezaji wa mradi wa Kukuza Matumizi ya Mkaa Mbadala, Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema wanaendelea kutoa elimu na mafunzo kwa watengenezaji mkaa mbadala na kuhamasisha umma umuhimu wa kutumia nishati hiyo.

Amesema mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2022 tayari umewafikia watengenezaji 59 katika mikoa 12 ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Mwanza, Tabora, Iringa, Dodoma na Zanzibar.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (REPOA), Dk. Donald Mmari, amesema kuna haja ya kuongeza ufanisi katika uzalishaji na kuhakikisha mkaa mbadala unapatikana kirahisi na wananchi wanafahamu faida zake kiuchumi na kiafya.

“Tulifanya utafiti kuangalia mkaa mbadala ni upi, gharama zikoje, upatikanaji wake na faida zake. Wananchi wengi hawafahamu sana na upatikanaji wake ni mdogo, uzalishaji wake una changamoto nyingi. Mafunzo yatasaidia kuongeza chachu ya matumizi ya mkaa mbadala, kupunguza uharibifu wa mazingira na kusaidia watumiaji kuepuka athari za kiafya,” amesema Dk. Mmari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (REPOA), Dk. Donald Mmari, akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi wa Kukuza Matumizi ya Mkaa Mbadala, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Dk. Mmari, mwaka 2015 upotevu wa misitu ulikuwa hekta 372,000 na hadi kufikia mwaka 2022 ulifikia hekta 469,120 akitahadharisha kuwa kuna hatari ya kuongezeka kwa ukame, jangwa na hewa ukaa.

Tafiti zinaonyesha Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na watengenezaji wengi huki watumiaji wengi wa nishati hiyo wakiwa ni wafanyabiashara ambapo umewasaidia kupunguza gharama kwa kuwa wanatumia kiwango kidogo kulinganisha na mkaa unaotengenezwa kwa kutumia kuni.

Related Posts