Afrika katika Magazeti ya Ujerumani – DW – 11.10.2024

die tageszeitung

Juma hili die tageszeitung liliangazia ajali ya boti iliyotokea juma lililopita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Limeandika kuwa wiki moja baada ya ajali hiyo mamlaka na ndugu waliofariki dunia katika ajali hiyo wako katika mtafaruku.

Katika ajali hiyo, boti ya “MV Merdi” ilizama siku ya Alhamisi wakati ilipokuwa ikiingia katika bandari ya Goma. Ilikuwa ikitokea katika mji mdogo wa Minova, na kulingana na watu walioshuhudia, ilikuwa imewabeba mamia ya watu. Operesheni kubwa ya uokoaji ilifanyika. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, watu 34 pekee walikufa maji na 80 waliokolewa.

die Tageszeitung limebainisha kuwa, takwimu hizo zimeibua maswali mengi kuhusu wengi wa abiria waliokuwa kwenye boti hiyo ambao wanatajwa kuwa wametoweka. Itakumbukwa kuwa siku yenyewe ya ajali kulikuwa na ripoti zilizodai kwamba watu 78 walikufa. Hata hivyo, kuna minong’ono inayozidi kushika kasi katika mji wa Goma kuwa, kuna miili mingi zaidi iliyoopolewa, lakini mamlaka zimeizuwia. Inahisiwa kuwa, ni kwa sababu serikali iliahidi kuwalipa fidia wafiwa na hivyo inataka kutaja idadi ndogo ya waliokufa kadri iwezekanavyo ili kuepuka kuingia gharama kubwa.

die tageszeitung, liliandika pia kuhusu mchakato wa kumuengua Naibu wa Rais wa Kenya Rigathi Gachagua uliokuwa gumzo kubwa nchini humo. Linaeleza kuwa, kwa miezi kadhaa, serikali ya Kenya ilipambana kujilinda dhidi ya maandamano ya vijana wenye hasira kali walioamua kuingia barabarani lakini safari hii, mapambano ni ndani ya serikali yenyewe.

Tangu Jumanne, juhudi zilianza kufanyika ili kuanza mchakato wa kumwondoa madarakani Naibu wa Rais. Baada ya hoja hiyo kufika bungeni, wabunge 281 kati ya 349 waliiunga mkono kiongozi huyo kuenguliwa. Mchakato wa kumwondoa madarakani sasa umefika katika Baraza la Seneti la Kenya. Gachagua anakabiliwa na tuhuma kadhaa zikiwemo matumizi mabaya ya ofisi, kukiuka katiba, kudhoofisha umoja wa kitaifa na kuchochea chuki za kikabila.

Anatuhumiwa pia kwa kujilimbikizia mali ambapo anadaiwa kuwa tangu ashike wadhifa wa naibu wa rais madarakani miaka miwili iliyopita hadi sasa ameshajikusanyia utajiri wenye thamani ya karibu euro milioni 36. Mali nyingi kati ya zinazounda utajiri huo ni hoteli wakati akipokea mshahara wenye thamani sawa na Euro 85,000 kwa mwaka.

Rigathi Gachagua
Naibu wa Rais wa Kenya Rigathi GachaguaPicha: picture alliance / NurPhoto

Die tageszeitung limeandika, Gachagua hata hivyo anakanusha tuhuma hizo akidai kuwa alirithi hoteli zinazotajwa na badala yake amerusha tuhuma lukuki kwa Rais William Ruto. Baadhi ya wafuasi wa Rais Ruto wanasema kuwa Gachagua aliyatumia hata maandamano makubwa ya vijana maarufu Gen Z yaliyoitikisa Kenya miezi ya Juni na Julai kumtaka Rais ajiuzulu.

Faz.Net

Gazeti la mtandaoni la Faz.Net liliyamulika maandalizi ya kampeni kubwa ya kutoa chanjo dhidi ya virusi vya mpox katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mwishoni mwa juma lililopita awamu ya kwanza ya dozi 265,000 za chanjo ziliwasili katika taifa hilo la Afrika ya Kati.

Licha ya hatua hiyo, Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mara moja ilitoa tamko kuwa dozi hizo za chanjo hazitoshi. Waziri wa Afya Samuel Roger Kamba alinukuliwa akisema kuwa, chanjo 265,000 haziwezi kutatua tatizo katika taifa lake lenye watu milioni 100. Nchi hiyo inatazamia kupokea chanjo nyingine zaidi kutoka Ufaransa, Japan na Marekani.

Itakumbukwa kuwa, mnamo mwezi Agosti, Shirika la Afya Duniani, WHO lilivitangaza virusi vya mpox kuwa dharura ya afya ya umma baada ya virusi hivyo kusambaa barani Afrika na baadhi ya visa kuripotiwa katika maeneo mengine duniani. Hata hivyo, bado Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inasalia kuwa kitovu cha maambukizi hayo ikiwa na asilimia 90 ya maambukizi ya virusi hivyo.

Zeit Online

Katika ripoti nyingine inayofanana na hiyo, majaribio ya chanjo dhidi ya virusi vya Marburg yameanza nchini Rwanda, ndivyo lilivyoandika gazeti la Zeit Online. Gazeti hilo la mtandaoni limemnukuu Waziri wa Afya nchini humo Sabin Nsanzimana akisema kuwa, dozi 700 za awali za chanjo hiyo zimetengwa kwa ajili ya wahudumu wa afya.

Chanjo dhidi ya virusi ya Marburg inafanyiwa majaribio Rwanda
Chanjo dhidi ya virusi ya Marburg inafanyiwa majaribio RwandaPicha: Depositphotos/IMAGO

Hadi sasa hakuna wasiwasi kuhusu madhara ya kiafya yanayoweza kuletwa na chanjo hiyo. Pamoja na ukweli huo, taasisi ya chanjo ya Sabine yenye makao yake nchini Marekani imetengeneza chanjo nyingine ambayo sasa inafanyiwa majaribio katika awamu ya pili nchini Rwanda. Majaribio kama hayo yanafanyika pia Uganda na Kenya ambako kwa mujibu wa watengenezaji hakuna wasiwasi wowote ulioripotiwa kuhusu usalama wa chanjo hiyo.

Majaribio hayo yanafanyika baada ya Rwanda kuutangaza mlipuko wa virusi hivyo vya Marbug Septemba 27. Takwimu rasmi za serikali ya nchi hiyo zinaonesha kuwa hadi sasa watu 46 wamepata maambukizi ya virusi hivyo wakati 12 kati yao walikufa. Juma lililopita, watu wawili mjini Hamburg nchini Ujerumani waliorejea kutoka Rwanda na kuhisiwa kuwa na maambukizi ya virusi hivyo walipimwa na kwa bahati nzuri hawakukutwa na maambukizi.

Inadhaniwa kuwa, virusi vya Marburg vinatokana na popo na vinaambukizwa kwa njia ya majimaji baada ya kugusana kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Baadhi ya dalili za maambukizi ya virusi hivyo ni pamoja na mtu kupata homa, maumivu ya misuli, kutapika na wakati mwingine kupoteza damu nyingi

Vyanzo: Deutsche Zeitungen

 

Related Posts