Mnada wakwanza wa Korosho wapata mafanikio Tandahimba na Newala,wakulima mashukuru rais Samia

Leo Oktoba 11, 2024, historia imeandikwa katika mikoa ya kusini baada ya kufanyika mnada wa kwanza wa korosho ulioandaliwa na Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (TANECU).

Katika mnada huo, jumla ya tani 3,857 za korosho zimeuzwa kwa bei ya juu ya shilingi 4,120 kwa kilo, huku bei ya chini ikiwa shilingi 4,035. Haya ni mafanikio makubwa kwa wakulima wa korosho ambao wamekuwa wakisubiri kwa hamu bei nzuri ya zao hili muhimu.

Wakulima wa Tandahimba na Newala wameonyesha furaha kubwa kwa hatua hii, huku wakimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake katika kuhakikisha bei za korosho zinapanda na kuwa na tija kwa wakulima. Wamesema kuwa mnada huu wa kwanza umewapa matumaini makubwa kwamba kilimo chao sasa kinaleta faida zaidi, na maisha yao yataboreka kutokana na ongezeko hili la kipato.

Akizungumza mara baada ya mnada huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Newala, mmoja wa wakulima wa korosho,alisema:

“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa juhudi zake za kuhakikisha tunapata bei nzuri kwa mazao yetu. Hii ni hatua kubwa kwa wakulima wa korosho, na tunaamini kwamba serikali itaendelea kutusaidia ili tuendelee kuuza kwa bei nzuri kama hii.”

Aidha, wakulima hao wameiomba serikali kuendelea kusimamia bei hizi kwenye minada ijayo, huku wakionyesha imani kwamba chini ya uongozi wa Rais Samia, sekta ya kilimo cha korosho itaendelea kuimarika na kutoa tija kwa wananchi wa mikoa ya kusini.

Mnada huu umeleta nuru mpya kwa wakulima ambao wamekuwa wakitegemea korosho kama chanzo kikuu cha mapato. Serikali imeonyesha dhamira thabiti ya kuimarisha bei za mazao ya kilimo, na hatua ya leo ni ishara tosha kwamba wakulima wanapewa kipaumbele ili kuinua uchumi wa mikoa ya kusini.

Meneja wa TANECU, Mohamedi Nassoro Mwinguku aliipongeza serikali kwa ushirikiano wake na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kuwa wakulima wanafaidika na mazao yao.

“Huu ni mwanzo mzuri kwa msimu huu wa korosho, tunatarajia kuona mafanikio zaidi katika minada ijayo. Tunaendelea kuwahimiza wakulima wetu kuongeza uzalishaji na kuzingatia ubora wa mazao yao,” alisema.

Hatua ya serikali ya kupandisha bei ya korosho ni miongoni mwa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kusisitiza kuwa serikali yake itaboresha maisha ya wakulima kwa kuhakikisha wanapata bei nzuri za mazao yao, hasa katika mikoa ya kusini kama Mtwara na Lindi.

Related Posts