Rais Mwinyi afungua S!te 2024, ampongeza Rais Samia ongezeko la watalii

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jitihada kubwa za kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii katika kipindi kifupi cha Serikali inayoongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Mwinyi amesema hayo wakati akifungua Onesho la 8 la Utalii la Kimataifa la Swahili (8th edition of the swahili international tourism expo – s!te 2024) lililoanza leo oktoba 11, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es salaam ambalo limewakutanisha wanunuzi wa bidhaa za utalii, Waoneshaji, Wawekezaji na wadau mbalimbali wa utalii wa ndani na nje ya Tanzania.

“Kutokana na juhudi hizo za Rais Samia, idadi ya watalii wa kimataifa wanaotembelea Nchi yetu imekua kwa kasi sambamba na ongezeko la mapato yatokanayo na sekta ya utalii. Mathalan, hadi kufikia mwezi Agosti, 2024 Tanzania imepokea jumla ya watalii wa kimataifa 2,026,378 ikiwa ni takwimu za juu kabisa kuwahi kufikiwa katika historia ya Nchi yetu. Pia, mapato yatokanayo na sekta ya utalii yamefikia Dola 3.5 bilioni,” amefafanua Mwinyi.

Dk. Hussein Ali Mwinyi

Amesema sekta ya utalii imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania, huku ikichangia asilimia 17.2 ya Pato ghafi la Taifa, asilimia 25 ya mauzo ya nje na kuzalisha ajira zaidi ya milioni 1.5 ikiwa ni ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia mnyororo wake wa thamani.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamewezesha nchi yetu kutambuliwa kimataifa na kupata tuzo mbalimbali ambapo taarifa iliyotolewa mwezi Septemba, 2024 na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism – World Tourism Barometer) ambapo inaonesha kuwa, Tanzania imeshika nafasi ya 6 Duniani na ya kwanza Barani Afrika kwa kuwa na ongezeko kubwa la watalii.

Miongoni mwa tuzo hizo ni zile zilizotolewa mwaka 2023 na World Travel Awards (WTA) ambao wameitambua Bodi ya Utalii Tanzania kama Africa’s Leading Tourist Board, Kisiwa cha Thanda Shunghumbili, Mafia kama World Leading Exclusive Private Island, Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kama Africa’s Leading Tourist Attraction, na Hifadhi ya Taifa Serengeti kama Africa’s Leading National Park. Aidha, mtandao wa Trip Advisor umezitambua Hifadhi za Taifa Serengeti na Tarangire kama Africa’s Top Attractions kwa mwaka 2023. Vilevile, Island Index wameitaja Zanzibar kuwa The 2nd Best Island Destination in the World kwa mwaka 2024.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana amesema wizara kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) itaendelea kutekeleza majukumu yake iliyopewa ya kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi sambamba na kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Utalii kwa kuzingatia Sera na miongozo mbalimbali.

Ametaja miongozo hiyo kuwa ni pamoja na Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999, mpango kamambe wa Utalii wa mwaka 2002, Ilani ya CCM kwa kipindi cha mwaka 2020 mpaka 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo, na Mkakati wa Kutangaza Utalii Kimataifa.

Amesema katika muktadha huo, mwaka 2014 Bodi ya Utalii Tanzania ilianzisha Onesho la Utalii la Kimataifa lijulikanalo kama Swahili International Tourism Expo (S!TE), lengo ni kuwakutanisha watoa huduma waliopo katika mnyororo wa thamani wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi ambao hupata fursa ya kuonesha bidhaa mbalimbali za utalii sambamba na kutengeneza mtandao wa kibiashara (Business Networking).Pia kuutangaza utalii wa Tanzania katika nyanja za kimataifa.

Amemshukuru Rais Samia kwa kusimama kidete kuufufua Utalii wa Tanzania uliokuwa umeathiriwa vibaya na janga la UVIKO-19 na kuzindua Programu ya Tanzania the Royal Tour ilichochea kuirejesha biashara za utalii katika hali yake ya awali na imeleta mafanikio makubwa katika Sekta.

About The Author

Related Posts