Ziara hii inafanyika huku mzozo unaotanuka wa Mashariki ya Kati na uhamiaji zikiwa mada zitakazojadiliwa, haya yamesemwa na maafisa wa Ujerumani Ijumaa.
Scholz atafanya mazungumzo na Erdogan Oktoba 19 mjini Istanbul,utakaofuatiwa na mkutano na waandishi wa habari, amesema msemaji wa serikali ya Ujerumani Wolfgang Buechner alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Berlin.
Mara ya mwisho Kansela Scholz kuizuru Uturuki ilikuwa Machi 2022, miezi michache baada ya kuingia afisini.
“Vita vya Ukraine na Mashariki ya Kati ndivyo vitakavyokuwa ajenda kuu kwenye mazungumzo hayo. Uhamiaji na masuala ya sera za nchi hizi mbili pia yatakuwa katika ajenda,” alisema Buchner.
Udikteta unaozidi
Uhusiano wa Ujerumani na Uturuki ni tete licha ya kuwa Ujerumani ni mwenyeji wa idadi kubwa ya Waturuki barani Ulaya.
Katika miaka ya hivi karibuni, maafisa wa Ujerumani wamelalamikia kinachoendelea Uturuki wakisema wanaona udikteta unaozidi chini ya Erdogan.
Kuzuka kwa vita vya Israel dhidi ya Hamas huko Gaza, kumeupelekea uhusiano huo kuvurugika zaidi.
Erdogan mara kadhaa ameishambulia Israel kutokana na vitendo vyake Gaza wakati ambapo Ujerumani inaiunga mkono pakubwa Israel na imeitetea haki ya Israel ya kujilinda, ingawa imetoa wito wa usitishwaji mapigano.
Chanzo: AFP