TUMUENZI HAYATI MWL. NYERERE KWA CHAGUZI ZA HURU NA HAKI


Farida Mangube, Morogoro

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Kighoma Malima amewataka watanzania kumuenzi Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa maono yake ya kuwa na uchaguzi huru na wahaki nyakati zote ili kulinda tunu ya umoja, amani na upendo aliyeiacha kiongozi huyu.

Rc Mlima amesema hayo wakati akifungua Kongamato la 21 la kumbukizi ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere lililoandaliwa na Chuo kikuu Mzumbe na kubeba kauli mbiu isemayo “Mtazamo wa Mwl. Nyerere juu ya dhana ya uchaguzi huru na wa haki”.

Amesema mtazamo wa Mwalimu kuhusu uchaguzi huru na wa haki si suala la kisiasa tu, ni suala la kulinda rasilimali watu ambayo kutoka miongoni mwao, wanapatikana viongozi na watendaji bora, watakao tunga sera na sheria bora zitakazo ongoza Taifa.

Aidha amekitaka Chuo Kikuu Mzumbe kuandaa watu wenye maadili na sifa nyingine za kiongozi bora ili kuwezesha uwepo wa utawala bora utakaotunza rasilimali za Taifa kwa maendeleo endelevu ya Taifa hili.

Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Pro. William Mwegoha amesema kwa miaka mingi, Chuo Kikuu Mzumbe tumekuwa na utaratibu wa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kufanya makongamano ya kitaaluma yanayojadili mitazamo tofauti ya Mwalimu Nyerere, ikiwemo utawala bora, mchango wa vyuo vikuu katika kuboresha kilimo biashara, na uchumi mzunguko kwa maendeleo ya Taifa,

Amesema Chuo Kikuu Mzumbe kwa mwaka 2024 imekuja na kauli “Mtazamo wa Mwalimu kuhusu Dhana ya Uchaguzi Huru na wa Haki.” ikiwa ni mahsusi nyakati hizi ambapo Taifa linakaribia kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa mwezi Novemba, na uchaguzi mkuu hapo mwakani 2025.



Related Posts