WAKUU wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mikoa (RCOs), wamejifungia jijini Dodoma kujadili na kujikumbusha wajibu wao katika kuihudumia jamii. Anaripoti Mwandishi Wetu, … (endelea).
Hayo yameelezwa leo tarehe 11 Oktoba 2024 na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Ramadhani Kingai, ambaye ni mwenyekiti wa kikao hicho.
DCI Kingai amesema lengo la kikao hicho, ni kujadili na kujifunza mambo yatakayoweza kuongeza weledi katika utendaji wao wa kazi za kila siku.
Amesema mada mbalimbali zitatolewa ikiwamo inayohusu wajibu wa Jeshi la Polisi, katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akifungua kikao hicho, Kamishna wa Uchunguzi wa Kisayansi, Kamishna wa Polisi, Shaban Hiki, amewapongeza wakuu hao wa upelelezi, kwa kazi kubwa wanayoifanya, inayoiwezesha Tanzania kuendelea kuwa shwari.
Kikoa hicho kinawahusisha Wakuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mikoa (RCOs) na pia Wakuu wa Vitengo vilivyopo Ofisi ya DCI, Makao Makuu ya Polisi Dodoma, wanashiriki.
“Watu wanaendelea na shughuli zao za uzalishajimali bila hofu hapa nchini na ninyi ni moja ya watu ambao mna mchango mkubwa katika hilo, hivyo, endeleeni kusimamia vyema masuala ya haki jinai katika maeneo yenu,” amesema Kamishna Hiki.