AIR FRANCE- KLM YATOA FURSA WASICHANA 20 KUTOKA VITUO VYA KULEA WATOTO YATIMA KUTEMBELEA JNIA

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, Wasichana ishirini kutoka Vituo vya kulea Watoto Yatima vya Shalom na Bulongwa wamepata fursa ya kutembelea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu usafiri wa anga,

Akizungumza katika ziara hiyo leo Oktoba 11, 2024 Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Air France-KLM nchini Tanzania, Rajat Kumar, alisema, “Wasichana vijana wanaishi katika mazingira magumu wanahitaji kupewa nafasi za kujifunza. Kwa kuleta ziara hii, tunatarajia kuwapa motisha ya kuona wenyewe katika nafasi za kazi zinazowezekana katika sekta ya usafiri wa anga.”

Aidha Kumar alisema Kampuni ya Air France-KLM inajitahidi kuimarisha ushiriki na uongozi wa wanawake katika sekta hiyo, ambapo takribani 44.6% ya wafanyakazi wake ni wanawake.

Alisema kampuni hiyo ina lengo la kuongeza uwiano wa wanawake katika kamati za usimamizi hadi 50% katika miaka ijayo.

Pamoja na hayo alisema waliamua kuchukua uamuzi wa kuwapeleka watoto hao katika uwanja wa ndege kwaajili ya kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatawapatia hamasa ya kujituma zaidi iliwaweze kufikia ndoto zao.

Kwa upande wa watoto hao waliushukuru uongozi wa Air France -KLM kwa kuwapatia nafasi hiyo adhimu kwani imewajengea moyo wa kupambana na kutokukata tamaa.













Related Posts