MASHABIKI  WA YANGA AMBAO NI ASKARI POLISI WA KIKE WATOA ZAWADI KWA WATOTO  JKCI

 

Mashabiki wa timu ya mpira ya Yanga ambao ni askari Polisi wa kike kutoka vituo mbalimbali vya Jeshi hilo vya mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mara baada ya kutoa zawadi za watoto wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

Mashabiki wa timu ya mpira ya Yanga ambao ni askari Polisi wa kike kutoka vituo mbalimbali vya Jeshi hilo vya mkoa wa Dar es Salaam wakiwajulia hali watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walipotembea taasisi hiyo leo kwaajili ya kutoa zawadi za watoto wenye matatizo.

Picha na JKCI

Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

 Mashabiki wa timu ya mpira ya Yanga ambao ni askari Polisi wa kike kutoka vituo mbalimbali vya Jeshi hilo vya mkoa wa Dar es Salaam wametoa zawadi  kwa watoto wenye matatizo ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya  Kikwete (JKCI) .

Zawadi hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na askari hao ambao walifika katika taasisi hiyo kwaajili ya na kutoa zawadi ambazo ni mahitaji ya kila siku ya watoto, kuwapa pole watoto pamoja na kuwafariji ndugu zao wanaowauguza.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadi hizo Mkuu wa Polisi wilaya maalumu ya kipolisi ya Mabwepande Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Colle Mashauri alisema wao kama wanawake wanatambua changamoto za watoto walioumwa pamoja na wazazi wao wanaowauguza hivyo basi wakaona ni vyema wafike katika taasisi hiyo kwaajili ya kuwafariji na kuwapa pole.

“Tumekuja kutoa msaada kwa watoto ikiwa ni mwendelezo wa kauli mbiu yetu ya  kuhakikisha watoto hawafanyiwi vitendo vya ukatili wa kijinsia isemayo tuwaambie kabla hawajaharibiwa, tuna madawati ya kupambana na ukatili wa kijinsia nchi nzima ambayo tunayatumia kuwasaidia watu wanaopitia katika changamoto hizo”.

“Ninawaomba wadau mbalimbali wakimemo mashabiki wa timu za mpira waige mfano wetu waje kuwaona watu wenye mahitaji mbalimbali kwa kufanya hivi watakuwa wamewafariji na kuonesha upendo kwao”, alisema SSP Colle.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alishukuru kwa zawadi hizo  na kusema kuwa zimekuwa ni faraja  kubwa kwa watoto na ndugu zao wanaowauguza.

“Ninashukuru sana kwa zawadi hizi watoto hawa kama mnavyowaona wanatoka katika mikoa  mbalimbali na wengine hawana ndugu hapa Dar es salaam wamefurahi kwa zawadi, ninawaomba watu wengine wafike hospitali  kuwasaidia watu wenye uhitaji”, alisema Dkt. Anjela.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi wenzake ambao watoto wao wamelazwa katika taasisi hiyo Zainabu Abdala mkazi wa Tandika alisema mtoto wake alilazwa katika wodi hiyo tangu mwezi wa nane mwaka huu na kufanyiwa upasuaji wa moyo mwezi wa tisa anamshukuru Mungu mtoto anaendelea vizuri na ameruhusiwa kurudi nyumbani.

“Binafsi nilikata tamaa kabisa kuhusu matibabu ya mwanangu ninawashukuru sana wauguzi na madaktari ambao wamempambania mwanangu ambaye amepona na leo hii ameruhusiwa kurudi nyumbani”,.

“Ninawashukuru wadau ambao mmekuwa mkitusaidia kwa namna moja au nyingine kwani watu mbalimbali wanakuja hapa wanatoa mahitaji ya watoto na kutupunguzia wazazi mawazo ya wapi tungepata mahitaji yao”, alisema Zainabu.

Zainabu aliwatia moyo wazazi ambao wana watoto wenye matatizo ya moyo wasikate tamaa kama yeye wasimame na Mungu kwani hakuna kisichowezekana kuna wataalmu wazuri wenye  moyo wa upendo na kujali ambao wanawahudumia watoto wenye matatizo ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Related Posts