Serikali yawahakikishia wawekezaji usalama na fursa za faida Tanzania

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Serikali imewahakikishia wawekezaji kwamba Tanzania ni sehemu salama kwa uwekezaji na ina fursa nyingi za kibiashara zenye faida. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, alitoa wito huu Oktoba 12, 2024, wakati akifungua mkutano wa jukwaa la uwekezaji katika sekta ya utalii.

Mkutano huu ulifanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, kama sehemu ya Onesho la 8 la Utalii la Kimataifa la Kiswahili (S!TE 2024).

“Kama mnavyofahamu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kufungua sekta ya utalii na kutangaza vivutio vya nchi yetu. Sasa tuna watalii wengi wanaokuja kutembelea, lakini tunahitaji pia wawekezaji kuboresha miundombinu, kama vile kuongeza idadi ya hoteli za kisasa,” alisema Kitandula.

Aliendelea kusema kuwa mkutano huo uliwaleta pamoja wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii ili kuwaelimisha kuhusu fursa zilizopo nchini. “Sekta ya utalii inachangia karibu asilimia 25 ya mapato ya kigeni, lakini bado kuna nafasi kubwa ya kuendelea kuvutia uwekezaji ili kuinufaisha zaidi kiuchumi,” alieleza.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, alisisitiza kuwa mkakati wa wizara ni kuzalisha na kutangaza mazao mbalimbali ya utalii na kuainisha fursa za uwekezaji. Mafuru alisema kuwa TTB imejipanga kuwaonyesha wawekezaji maeneo mbalimbali yenye fursa za kipekee katika kusini, magharibi, pwani ya mashariki, na Zanzibar.

“Katika S!TE, tumewaalika wawekezaji kuona fursa katika mazao ya utalii kama utalii wa fukwe, mikutano, na michezo. Kuna mazao mengi yanayoweza kuvutia uwekezaji wa kimataifa,” alisema Mafuru.

Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa Hoteli ya Dar es Salaam Serena, Seraphin Lusala, aliongeza kuwa kuna haja ya kuongeza hoteli zenye hadhi ya kimataifa nchini. Alisema kuwa ongezeko la watalii linaenda sambamba na mahitaji ya hoteli nyingi zaidi.

“Mji kama Dar es Salaam unahitaji kumbi kubwa za mikutano na vyumba vya kulala vya kutosha. Serikali inapaswa kuhamasisha uwekezaji katika sekta hii ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka,” alisema Lusala.

Alisema kuwa ili kuleta wawekezaji wengi zaidi, ni muhimu kuwapa elimu kuhusu faida na motisha zinazotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ambazo zitawavutia zaidi kuwekeza kwenye sekta ya hoteli.

Related Posts