Waziri Mhagama ampongeza Haroon kwa uwekezaji wa hospitali ya Shifaa

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Afya, Jenista Mhagama amezindua Kituo cha Tiba na Utafiti wa Saratani cha Shifaa na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuongeza bajeti ya dawa za saratani kila mwaka kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani.

Waziri Mhagama aliyasema hayo Ijumaa jioni jijini Dar es Salaam wakati akizindua kituo hicho kilichoko kwenye hospitali ya Shifaa barabara ya Msese Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alisema wakati idadi ya wagonjwa ikiongezeka wagonjwa wengi wanaougua ugonjwa huo hawana uwezo wa kugharamia matibabu hivyo wanahitaji kusaidiwa.

Alisema kwa mwaka huu wa fedha pekee serikali imetenga shilingi bilioni 10 kwaajili ya kununua dawa za saratani na kwamba kila bajeti mpya kiasi hicho kitakuwa kikiongezeka.

Alisema uwepo wa kituo hicho utaongeza upatikanaji wa huduma muhimu sana za kiuchunguzi na kitabibu kwa matatizo yanayohusu ugonjwa wa saratani nchini.

Alisema saratani imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na takwimu za kila mwaka zinaonyesha kuwa na ongezeko na mwaka 2022 wagonjwa wapya wa saratani walikuwa 45,000.

“Wagonjwa wa saratani wasipowahi kupata matibabu inawasababishia vifo kwa hiyo unapokuwa na wagonjwa 45,000 nchi lazima iweke mipango ili kuokoa uhai wa wananchi hao kwa kupata tiba mapema,” alisema

Alitaja saratani zinazoongoza kuwa ni saratani ya mlango wa kizazi inayochukua asilimia 24.2, saratani ya tezi dume inachukua asilimia 10.7, saratani ya matiti inayochukua asilimia 10, saratani ya koo inayochukua asilimia 7.9, saratani ya utumbo mpana inayochukua asilimia 4.9 ya aina zote za saratani nchini.

Waziri Mhagama alisema saratani zote hizo zinachukua asilimia 42 ya idadi ya wagonjwa wote wanaougua saratani nchini na saratani zinazoathiri zaidi wanawake nchini ni ile ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti.

“Ndiyo maana serikali imeamua kuchukua jitihada za kukinga wananchi wake dhidi ya saratani na pale ambapo mtu anapata saratani apate matibabu na leo Shifaa wanapounga mkono juhudi za serikali kuokoa wagonjwa wa saratani na kuwarejeshea furaha tunawashukuru sana,” alisema Mhagama.

Alisema serikali imeendelea kutoa elimu na kufanya kampeni maalum za uchunguzi na utambuzi wa mapema wa maradhi ya saratani na kupanua huduma za uchunguzi kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Alisema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na vituo vingi vya utoaji wa huduma hizo na hasa kwa wanawake na serikali imeimarisha huduma za uchunguzi a kimaabara na huduma za radiolojia kwa kuhakikisha inakuwa na mashine 85 za CT SCAN za kutosha na MRI.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Shifaa, Bashir Haroon aliipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa inaofanya kwenye sekta ya afya.

Alisema hospitali ya Shifaa ni uwekezaji ambao umegharimu dola za Marekani milioni 60 kama jitihada za kuwawezesha wananchi kupata matibabu bora yanayokwenda na wakati.

“Ujenzi wa hospitali hii umefanywa kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali katika sekta ya afya na tunafurahi kuona maboresho makubwa yakiendelea kwenye sekta ya afya na navipongeza vituo binafsi vya afya kwa kazi kubwa wanayofanya,” alisema

Haroon alisema ugonjwa wa saratani umekuwa tatizo kubwa sana duniani na hapa Tanzania na ndiyo sababu yeye aliona umuhimu wa kuanzisha kituo cha tiba ya saratani ili kuwapunguzia mzigo wa gharama wagonjwa wa Tanzania wanaokwenda India kutibiwa.

Related Posts