Aliyekuwa waziri wa fedha na masuala ya ajira na gavana wa kwanza mweusi wa benki kuu nchini Afrika Kusini Tito Mboweni amefariki Jumamosi usiku akiwa na umri wa miaka 65.
Mboweni alikuwa mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi wakati alipokuwa mwanafunzi na baadae alikuja kuwa waziri wa leba wa kwanza katika Afrika Kusini ya kidemokrasia kuanzia mwaka 1994 hadi 1999 chini ya rais wa zamani Nelson Mandela.
Kuanzia mwaka 1999 aliitumikia nchi hiyo kama gavana wa benki kuu kwa kipindi cha muongo mmoja na baadae kushikilia wadhifa wa waziri wa fedha kuanzia 2018 hadi 2021 chini ya utawala wa rais Cyril Ramaphosa.
Chama cha African National Congress, ANC kimemuelezea Mboweni kama sauti iliyoaminika katika mijadala iliyohusu masuala ya kiuchumi, iliyojenga kipindi cha baada ya kuingia kwenye demokrasia.
Dhima ya kiongozi huyo katika kujenga mustakabali wa demokrasia ya Afrika Kusini na hasa wakati wa ubaguzi wa rangi haiwezi kusahaulika kwa mujibu wa ANC.
Kwa mujibu wa chama hicho, Mboweni alisaidia kuanzia sheria ya usimaizi wa masuala ya ajira katika kipindi cha baada ya utawala wa ubaguzi wa rangi ambayo iliweka msingi wa kuwepo mahakama za kutetea haki za wafanyakazi.Soma pia: Je, unafahamu namna Baraza la mawaziri la Afrika Kusini lilivyogawanywa?
Lakini pia kama gavana wa benki kuu alisimamia hatua ya kupanda kwa mfumuko wa bei iliyolenga kuisadia benki hiyo kuleta uthabiti wa viwango vya bei.
Alikuwa mshirika wa karibu wa Ramaphosa na alitumikia kamati kuu ya chama cha African National Congress,chombo ambacho kinahusika kutowa maamuzi ya chama.
Rais Ramaphosa amesema kutokana na umuhimu wa Mboweni na juhudi zake katika ushirikiano na waafrika Kusini wenzake,kufariki kwake akiwa na umri wa miaka 65 ni jambo lililowashtuwa.
Taarifa ya rais Ramaphosa imesema Afrika Kusini imepoteza kiongozi na mzalendo aliyeitumikia kama mwanaharakati,mbunifu wa sera za uchumi na bingwa wa kutetea haki za masuala ya ajira.