Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair leo Jumapili aliungana na mfalme Charles III miongoni mwa watu wengine mashuhuri nchini humo, kutowa heshima zao kwa aliyekuwa waziri kiongozi wa Scotland Alex Salmond aliyefariki ghafla akiwa na umri wa miaka 69.
Tony Blair amesema amesikitishwa sana aliposikia taarifa za kifo cha kiongozi huyo na kuongeza kwamba, pamoja na kutofautiana kwake na Salmond, alikuwa kiongozi mkubwa katika siasa za Scotland na Uingereza na hapana shaka aliitumikia Scotland na watu wake kwa dhati kabisa.
Alex Salmond alikuwa ni mwanasiasa, na kiongozi aliyepambania vuguvugu la kudai uhuru wa Scotland na pia kiongozi wa chama cha Scottish National Party SNP kwa miaka 10 aliyowahi kuwa waziri kiongozi, alifariki Jumamosi huko Macedonia ya Kaskazini.
Vyombo vya habari nchini Uingereza vimeripoti kwamba Salmond aliyeiongoza Scotland kati ya mwaka 2007 na 2014 aliugua ghafla baada ya kutowa hotuba.
Itakumbukwa kwamba safari yake ya kisiasa iligubikwa na panda shuka nyingi, akishuhudia ndoto zake za kuiona Scotland inapata uhuru zikizimwa mara kadhaa huku akishuhudia mivutano na mipasuko ya mara kadhaa ikiwemo na mshirika wake wa zamani Nicola Sturgeon, aliyekuja kumrithi nafasi ya waziri kiongozi wa Scotland.
Lakini wafuasi wake na wanaomkosoa wanamtambuwa kama mwanasiasa ambaye hakuogopa athari za hatua zake na alikuwa mwenye maarifa, akisifika kwenye nyanja mbali mbali.
Kwa kiasi kikubwa akionekana kuwa mmoja wa wanasiasa wenye uwelewa mkubwa wa mambo na haiba katika enzi hizi. Salmond alikibadili chama cha SNP kutoka kuwa chama kidogo katika bunge la Uingereza na kukifanya kuwa nguvu kubwa ya kisiasa iliyoihodhi Scotland.
Na haiba yake ya kuwa mpambanaji iliufanya umaarufu wake kuvuka hata mipaka ya Uingereza. Mvutano wake na Donald Trump ulimfanya rais huyo wa zamani wa Marekani kumpachika jina la ”Alex kichaa”.
Mfalme Charles wa III baada ya kupokea taarifa za kifo cha waziri huyo Kiongozi wa zamani wa Scotland, Jumamosi usiku amesema amesikitishwa sana na kifo hicho cha bwana Salmond, akisema utiifu wake kwa Scotland ulioonekana katika kuutumikia umma wake huo kwa miongo kadhaa.Soma pia: Hatma ya Uingereza yaamuliwa Scotland
Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer ambaye amemtaja Salmond kama mtu aliyekuwa na umuhimu wa kipekee kwa siasa za Scotland na Uingereza anayeacha sifa itakayodumu.
Ikumbukwe kwamba Salmond alijiuzulu kama waziri kiongozi wa Scotland baada ya kushindwa kwenye kura ya maoni aliyoiongoza ya kudai uhuru wa eneo hilo na kujiondowa kwenye chama cha SNP mnamo mwaka 2018 kufuatia tuhuma za kuhusika na ubakaji na unyanyasaji kingono.Soma pia: Glasgow, Scotland. Chama kinachotaka uhuru chapata ushindi.
Alifutiwa mashtaka yote 14 yaliyomuandama katika kesi iliyofunguliwa mwaka 2020 na kulipwa dola 653,000 kama fidia kutoka serikali ya Scotland kutokana na namna ilivyoendesha uchunguzi juu ya suala hilo.Baadae alikuwa kiongozi wa chama kipya cha kupigania uhuru cha Alba lakini chama hicho kilishindwa kupata umaarufu na mafanikio ya Kisiasa kama SNP.
Chama chake hicho cha zamani SNP bado kinamtaja kama mwamba wa vuguvugu la kudai uhuru na hata waziri kiongozi wa sasa wa Scotland na kiongozi wa SNP John Swinney anasema Alex alifanya kazi bila kuchoka na kuipambania nchi aliyoipenda na uhuru wake.