Marekani kupeleka askari wake Israel – DW – 14.10.2024

Wizara ya ulinzi ya Marekani imetangaza kuwa itapeleka huko Israel wanajeshi pamoja na mifumo ya hali ya juu ya ulinzi wa anga, wakati huu serikali ya mjini Tel-Aviv ikijiandaa kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya Iran.

Kufuatia kauli hiyo, Iran imesema hivi leo kuwa kwa sasa haioni sababu za kuendeleza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani kwa upatanishi wa Oman kutokana na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati. Mwezi Juni, Tehran ilisema kuwa tayari kwa hatua hiyo licha ya kuwa nchi hizo mbili hazina uhusiano wowote wa kidiplomasia.

Soma pia: Marekani yaionya Israel kuhusu uharibifu Lebanon

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi yupo nchini Oman kama sehemu ya ziara yake ya kikanda ambapo alikutana na washirika wa madola ya Mashariki ya Kati.

Iran: Tuko tayari kwa vita lakini tunatoa kipaumbele kwa diplomasia 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi Picha: Mehr

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Esmail Baghaei amesema Araghchi amefanya pia mazungumzo na mwenzake wa Oman Badr Albusaidi kuhusu vita vinavyoendelea  Gaza na Lebanon , huku Araghchi akitoa wito wa kusitishwa kwa mzozo huo.

“Hatutaki vita ingawa tumejiandaa kikamilifu kwa vita. Tunafikiri kwamba diplomasia inapaswa kufanya kazi na kuzuia mgogoro mkubwa sana katika kanda hii.”

Araghchi amekutana na Mohammed Abdel Salam, ambaye ni afisa mkuu kundi la wahouthi wanaoungwa mkono na Tehran huko nchini Yemen. Kabla ya kuelekea Oman, Araghchi alikuwa mjini Baghdad kwa mazungumzo na maafisa wa Iraq na wiki iliyopita, aliizuru Qatar na Saudi Arabia.

Hayo yakiarifiwa, maafisa wa afya wa Lebanon wamesema watu 18 wameuawa leo Jumatatu kufuatia  shambulio la anga la Israel kwenye jengo la ghorofa katika kijiji cha Aito kusini mwa Lebanon. Israel imesema pia kuwa imemuua kamanda wa kikosi maalum cha Hezbollah Muhammad Kamel Naim kufuatia shambulio katika eneo la Nabatieh kusini mwa Lebanon. Hayo yanajiri baada ya Hezbollah kuwaua jana usiku askari wanne wa Israel baada ya kuvurumisha makombora kadhaa eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.

(Vyanzo: DPAE, AP, Reuters, AFP)

Related Posts