WAZAZI WAASWA KUTOA USHIRIKIANO KUKOMESHA VITENDO VYA UKATILI KWA WATOTO

 

Picha wakati wa Maandamano ya kupinga ukatili kwa watoto na watoto wa kike yaliyofanyika kata ya Bunju jijini Dar es Salaam.

Afisa ustawi wa Jamii Kata ya Bunju, Lilian Chillo akizungumza wakati wa maandimisho ya mtoto wa kike yaliyofanyika kata ya Bunju jijini Dar es Salaam.

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

OFISA Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Kinondoni Dar es Salaam Furaha Dibango amewataka wazazi nchini kutoa ushirikiano dhidi ya ukatili wanaofanyiwa watoto ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kwa haraka.

Amesema Manispaa hiyo inashirikiana na wadau mbalimbali kupambana na ukatili lakini juhudi hizo zinakwamishwa na baadhi ya wazazi na walezi ambao mara nyingi wamekuwa hawafiki kutoa ushahidi pindi wanapohitajika

Furaha amesema hayo leo Oktoba 14, 2024 wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani huko Bunju jijini Dar es Salaam ambapo kwa namna ya Pekee ambapo Shirika la Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI) wameandamana pamoja na madereva wa vyombo mbali mbali vya usafiri na kutoa matangazo wakiwa na kauli mbiu ‘Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono nawezekana’.

“Tumekuwa tukishirikiana na wadau mbalimbali kupambana na ukatili kwa watoto wa kike na sasa wakiume pia wanaingia wakiwamo WAJIKI, lakini juhudi hizo zinakwamishwa na baadhi ya wazazi na walezi kwani unakuta taarifa za ukatili zinatolewa, tunafuatilia na kubaini ukweli na kufikisha matukio katika vyombo vya sheria, lakini wazazi wanapoitwa kuja kutoa ushahidi hawajitokezi na badala yake, wanamalizana na wahalifu jambo ambalo linakwamisha vita ya rushwa ya Ngono.

Maadhimisho hayo yaliyoambatana na mwendelezo wa awamu ya sita ya kampeni ya ‘Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono’ Inawezakana’, yaliandaliwa na Shirika la Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI) na kufanyika Bunju A.

Mkurugenzi wa WAJIKI, Janeth Mawinza amesema wameanza awamu ya sita ya kampeni ya ‘Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono’ ambayo itadumu kwa miaka miwili.

“Wafadhili wetu, Women Fund Tanzania Trust (WFT), wametuwezesha Sh. milioni 800 kwa ajili ya kampeni hii ambapo tumeongeza kata tatu za Bunju, Tandika na Kitunda,” amesema Janeth.

Amefafanua kuwa wakifanya kampeni kwenye baadhi ya kata za wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke ambazo zimekuwa na mafanikio makubwa na kwamba awamu ya sita wameongeza kata hizo tatu lengo likiwa ni kuifikia Dar es Salaam yote na baadae kufika mikoani pindi wakipata uwezo zaidi wa kifedha kwani tatizo la rushwa ya ngono liko kila mahali.

Lengo letu kama tutapata uwezo zaidi wa kifedha, ni kuimaliza Dar es Salaam yote na kisha kwenda mikoani ambao ninaamini Kuna tatizo la rushwa ya ngono’ ” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU), mkoa wa Kinondoni, Bibie Msumi anasema, mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika vita vya ukatili wa kijinsia ni mkubwa.

“Kwa sasa jamii imepata uelewa wa kutosha kupitia elimu inayotolewa na mashirika hayo, wamekuwa walitoa taarifa za matukio ya rushwa ya ngono ambazo zinatusaidia katika majukumu yetu,” amesema Bibie.


Maandamano akiendelea

Baadhi ya wakazi wa kata ya Bunju wakichangia mada mara baada ya kupata elimu juuu ya kumlinda mtoto wa kike.

Related Posts