Bashungwa aongoza uhamasishaji wananchi kujiandikisha daftari la wapiga kura

Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ameongoza zoezi la uhamasishaji kwa Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kuendelea kujitokeza katika vituo vya kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura ili waweze kutimiza haki yao kikatiba ya kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024.

 

Bashungwa ameongoza uhamasishaji huo leo tarehe 15, Oktoba, 2024 mara baada ya kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura katika Kituo cha Ahakishaka Kata ya Nyabiyonza Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera ambapo zoezi hilo lilianza rasmi tarehe 11 Oktoba, 2024 na litamalizika tarehe 20 Oktoba, 2024.

 

“Nichukue nafasi hii kupaza sauti kwa kile ambacho Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wengine wameendelea kusisitiza wananchi kujitokeza kwa ajili ya kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, Nendeni mkajiandikishe na tuwakumbushe wenzetu ambao bado hawajajiandikisha kufanya hivyo kwa siku zilizobakia“, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kudumisha umoja na mshikamano kwa kuwa ndio msingi wa kuleta maendeleo katika Vijiji na kata zote za Wilaya ya Karagwe.

 

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imetoa kiasi cha Shilingi Milioni 647 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya katika katika ukanda wa Bushangaro ambacho kitajengwa Ahakishaka.

“Kama mnavyofahamu Wilaya ya Karagwe ina tarafa tano (5) na tayari tarafa ya Nyaishozi, Bugene, Kituntu zimeshapata vituo vya afya na sasa ni zamu ya Nyabiyonza, kituo cha afya kinajengwa na fedha zishaletwa na kwa tarafa ya Nyakakika mipango inaendelea”. ameongeza Bashungwa.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Kufa na Kuzikana (Tupendane) ya Ahakishaka Kata ya Nyabiyonza, Bw. Festo Mtele amemshukuru Mbunge kuungana na wananchi wa Wilaya ya Karagwe kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura na kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha ili kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa.

 

Related Posts