HAKUNA VITUO BANDIA VYA KUANDIKISHA WAPIGA KURA – MHE. MCHENGERWA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu uwepo wa vituo bandia vya kuandikisha wapigakura wa Serikali za Mitaa sio za kweli na taarifa sahihi ni kuwa alifafanua kuwa uandikishaji unafanyika kwenye vituo 80,812 kutokana na kuwa kuna baadhi ya mitaa au vitongoji vina vituo zaidi ya kimoja.

Ifahamike kuwa kwa Mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 796 na 797 kuhusu orodha ya maeneo yatakayoshiriki uchaguzi yanajumuisha jumla ya mitaa na vitongoji 68,543 lakini vituo vilivyopo ni 80,812 Lengo la kuwa na vituo hivi ni kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa ili kupata haki yao ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa.

Hii ina maana vipo vitongoji na mitaa ambayo inakituo zaidi ya kimoja na hii imefanyika miaka yote ya uchaguzi kutokana na wingi wa watu, jiogarafia ya mahali ya eneo husika mfano misitu au wananchi wana shughuli za kiuchumi katika maeneo ya wafugaji, wakulima, wachimbaji migodini au wananchi wanaishi mbali na Kituo cha uandikishaji hivyo kwa pamoja wasimamizi na viongozi wa vyama wanakubalina kuongeza kituo ili kuwafikia wananchi wote.

Aliongeza kuwa Kutowafikishia wananchi fursa ya kuwa na kituo ni kuwanyima haki yao ya kikatiba.

Suala la msingi pale inapobainika uhitaji wa kituo cha kuandikisha na kupiga kura, Kanuni zinaelekeza vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi katika eneo husika kukubaliana na kuamua ni wapi kituo kiwekwe ili kuhakikisha wananchama wao na wananchi wengine wote wanapata fursa hii ya kikatiba pasipo na kikwazo.

Waziri Mchengerwa ameyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari Jijini Mwanza leo tarehe 15.10.2024 kufafanua hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wadau wa uchaguzi hususan ni kipindi hiki cha uandikishaji.

Pia amewataka wadau wa vyama pamoja na wasimamizi wa uchaguzi/wasimamizi wasaidizi kukubaliana maeneo yote ambayo ni muhimu kukawa na vituo kwa nia ya kuwafikia wananchi wote pasipo na vikwazo.

Related Posts