Iran yalaani vikwazo vipya dhidi yake – DW – 15.10.2024

Umoja wa Ulaya na Uingereza umewawekea vikwazo watu saba na pia mashirika saba, likiwemo shirika la ndege la Iran kwa kuhusika na usafirishaji wa makombora ya masafa marefu ya Iran kwenda Urusi.

Mwezi uliopita, Marekani, ilinukuu taarifa za kijasusi ambazo ilisema imewapelekea pia washirika wake, kwamba Urusi ilikuwa imepokea makombora kutoka Iran, kuisaidia katika vita vyake nchini Ukraine.

Soma Zaidi:  Marekani kupeleka askari wake Israel

Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei, katika chapisho lake kwenye mtandao wa X siku ya Jumanne amekanusha vikali kwamba Iran imeipa Urusi makombora ya masafa marefu.

Iran | Esmaeil Baghaei
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil BaghaeiPicha: Khabaronline

Baghei ameongeza kusema kuwa baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya na Uingereza zinatoa madai bila ushahidi kuwa Iran inaingilia kati kijeshi mzozo wa Urusi na Ukraine. Ameeleza kwamba vikwazo hivyo vipya vinavyowalenga watu binafsi na mashirika ya Iran ni hatua inayokwenda kinyume na sheria za kimataifa.

Katibu mkuu wa chama cha mashirika ya ndege ya Iran, Maqsoud Assadi Samani, amesema  “Hakuna ndege ya Iran itakayosafiri kwenda Ulaya,” kufuatia vikwazo hivyo vipya.

Shirika la ndege la Iran linalomilikiwa na serikali lilikuwa ni mojawapo ya mashirika machache ya ndege yaliyofanya safari za moja kwa moja kutoka Ulaya kwenda Iran.

Tukigeukia kwenye mzozo wa mashariki ya kati, Marekani imewasilisha nchini Israel awamu ya kwanza ya mifumo ya kuzuia makombora, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Jenerali Pat Ryder, amesema katika siku zijazo, wanajeshi wa ziada wa Marekani watapelekwa nchini Israel na betri za mifumo ya THAAD pia vitafikishwa nchini humo.

Mfumo wa kisasa kabisa wa ulinzi wa anga unakusudiwa kusaidia kuilinda Israel kutokana na uwezekano wa mashambulizi ya anga ya Iran huku kukiwa na hofu ya kuzuka vita vya kikanda kwenye eneo la Mashariki ya Kati.

Marekani | Mfumo wa ulinzi wa anga aina ya THAAD
Mfumo wa kisasa kabisa wa ulinzi wa anga aina ya THAAD kutoka MarekaniPicha: Choo Sang-chul/Newsis via AP/picture alliance

Wakati huo huo mivutano ya kimadhehebu ya dini inaongezeka nchini Lebanon. Waislamu wengi wa madhehebu ya Shia wamelazimika kuhama kutoka kwenye maeneo yao ya kusini mwa Lebanon kwa ajili ya kuvikimbia vita, wenzao ambao ni wakaazi katika mji wa Wakristo katika upande huo wa kusini wana wasiwasi kuhusu kuwakaribisha walebanon wanaokimbia vita, wameelezea kuwa wanahofia huenda miongoni mwa wakimbizi hao wa ndani, wanaweza kuwemo wapiganaji wa Hezbollah watakaosababisha mashambulizi kutoka Israel.

Viongozi wa Lebanon ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa muda, Najib Mikati, mfanya biashara na Mwislamu wa madhehebu ya Sunni amesisitiza juu ya umuhimu wa kudumisha amani kwa raia wote wa Lebanon bila jukaji madhehebu ya dini zao.

Soma Zaidi: Israel yasema ‘maslahi ya taifa’ kwanza katika kuijibu Iran

Na Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na vita unakabiliwa na hali mbaya zaidi ya kushindikana kufikishwa misaada tangu vita vya Israel na Hamas vilipoanza zaidi ya mwaka mmoja.

Ukanda wa Gaza | Chanjo ya Polio
Mtoto akipewa chanjo ya Polio katina eneo la Khan Yunis katika Ukanda wa GazaPicha: Hani Alshaer/Anadolu/picture alliance

Umoja wa Mataifa umelalamikia athari mbaya zaidi inayowakabili watoto. Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF James Elder, amesema kila siku ifikapo, hali za watoto zinazidi kuwa mbaya zaidi kuliko siku iliyotangulia. 

Licha ya kuwepo haja kubwa ya kuongeza kiasi cha misaada inayoingia katika Ukanda wa Gaza, Elder ameeleza kuwa njia za kufikisha misaada hiyo hazipo.

Vyanzo: AFP/DPA

 

Related Posts