Mbeya, Tanga kuzalisha tani milioni 4 za saruji

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Upatikanaji wa saruji nchini unatarajiwa kuongezeka kutokana na upanuzi wa kiwanda cha saruji Mbeya na ujenzi wa kiwanda kipya jijini Tanga vitakavyozalisha tani milioni 4.2 kwa mwaka.

Hatua hiyo inafuatia baada ya Serikali ambayo inamiliki Mbeya Cement kwa asilimia 25 ya hisa na NSSF asilimia 10 kushirikiana na mbia mwenza Amsons Group kufunga mtambo mkubwa kwenye kiwanda hicho wenye uwezo wa kuzalisha malighafi (clinker) za kutengeneza saruji tani 5,000 kwa siku kutoka tani 1,000 za sasa.

Akizungumza leo Oktoba 15,2024 Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, amesema Serikali itashirikiana na mbia huyo kujenga kiwanda kipya jijini Tanga kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha malighafi (clinker) za saruji tani 5,000 kwa siku.

“Mahitaji ya saruji nchini ni makubwa kutokana na ujenzi wa miundombinu na uwekezaji unaofanywa na Serikali, wawekezaji wakiongezeka bei ya saruji itapungua.

“Tunakwenda kufanya uwekezaji mkubwa ili kukamata vizuri soko la Tanzania na soko la nchi jirani kama vile Zambia, Malawi na DRC. Tumeshafanya maamuzi ya msingi tunakwenda kuwekeza na baada ya miaka miwili au mitatu tutakuwa katika hatua nzuri,” amesema Mchechu.

Mkurugenzi wa Fedha kutoka Mbeya Cement, Ahmed Mhada, amesema uwekezaji katika Kiwanda cha Mbeya utagharimu Dola za Marekani milioni 130 wakati kwa Kiwanda cha Tanga utagharimu Dola milioni 190.

Amesema kupitia uwekezaji huo gawio litaongezeka zaidi ya mara kumi na ajira 12,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zitapatikana.

Related Posts