Mradi wa Umeme wa JNHPP mbioni kuzalisha Megawati 900

Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Serikali imeeleza kuwa Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) sasa una uwezo wa kuzalisha megawati 700 za umeme, na kwamba ndani ya kipindi kifupi kijacho, mradi huo utaweza kuzalisha hadi megawati 900.

Akizungumza leo Oktoba 15, 2024, jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya umeme na nishati jadidifu, Dk. Khatibu Kazungu, amesema mradi huu utasaidia kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini, huku akiainisha mipango ya serikali katika kuongeza vyanzo vingine vya nishati mbadala.

“Tanzania tuna uwezo mzuri wa kuzalisha umeme na sasa tunaangalia jinsi ya kuongeza megawati kupitia vyanzo vingine vya nishati kama vile mfumo wa jua, ambao kwa sasa unazalisha megawati 600, na jotoardhi, ambalo linaweza kutoa hadi megawati 5000,” alisema Dk. Kazungu.

Aidha, Dk. Kazungu alitaja pia mradi mwingine unaoitwa Gridi Imara, ambao unalenga kuboresha miundombinu ya umeme ili kuhakikisha huduma ya nishati inawafikia wananchi nchi nzima. Mradi huu pia unajumuisha mpango wa kuimarisha vyanzo vya umeme na kuongeza usalama wa nishati kwa taifa.

Kuhusu mkutano na wadau wa umeme wa Kanda ya Kusini mwa Afrika uliofanyika leo, Dk. Kazungu alisema kuwa lengo ni kuimarisha ushirikiano wa kanda hiyo katika kufua, kusafirisha, na kusambaza umeme kwa wateja wa kanda.

Alifafanua kuwa ushirikiano huo unahusisha pia mradi wa kuunganisha miundombinu ya umeme kati ya Tanzania na Zambia, ujulikanao kama TAZA, unaolenga kuimarisha mtandao wa usambazaji umeme katika kanda hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Costa Rubagumya, alisema kuwa ushirikiano kati ya nchi za SADC ni muhimu katika kuhakikisha kuwa upatikanaji wa nishati ni salama na endelevu.

“Faida kubwa ya ushirikiano huu ni kwamba nchi moja inaweza kusaidia nchi nyingine pindi inapokutana na changamoto katika upatikanaji wa umeme. Hili linatupa fursa ya kuwa na usalama wa nishati,” alisema Rubagumya.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wadau wa Umeme wa Kanda ya Kusini mwa Afrika, Steven Diwa, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kikanda ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati kwa nchi zote za kanda. Alibainisha kuwa ushirikiano huo unakuja wakati ambao Tanzania imepiga hatua kubwa katika miradi ya kuunganisha umeme na majirani zake, ikiwemo Kenya na Zambia.

“Tunaangazia mradi wa Julius Nyerere na mchango wake mkubwa kwa upatikanaji wa nishati katika kanda. Mradi huu sio tu kwamba utaongeza mapato ya Tanzania, bali pia utasaidia Tanesco kujifunza zaidi kuhusu uendeshaji wa mifumo mikubwa ya umeme iliyounganishwa,” alieleza Diwa.

Mkutano huo umeleta matumaini ya kuona Tanzania ikichangia kwa kiasi kikubwa katika mtandao wa umeme wa kikanda, ambao utaboresha upatikanaji wa nishati na kuleta manufaa kwa nchi zote wanachama wa SADC.

Related Posts