Katika taarifa, polisi ya taifa nchini Haiti imesema kamanda wa pili wa genge la Kraze Baryè, anayejulikana kama “Deshommes,” alipigwa risasi huko Torcelle, eneo linalodhibitiwa na genge hilo kusini mashariki mwa mji mkuu Port-au-Prince.
Wanachama 20 wa genge la Kraze Baryè nchini Haiti wauawa
Maafisa wa polisi wamesema kuwa wanachama wengine 20 wa genge hilo waliuawa wakati wa operesheni zilizofanywa siku ya Jumamosi na Jumatatu, na kuongeza kuwa walinasa bunduki, risasi, simu pamoja na vifaa vingine.
Polisi imesema msako huo utaendelea hadi genge hilo na kiongozi wake mkuu Vitel’Homme Innocent, litakapodhibitiwa.
Katika taarifa, polisi ya Kenya inayoongoza ujumbe huo wa Haiti, imetoa wito kwa Innocent kukoma kufanya ukatili dhidi ya raia wa Haiti wasiokuwa na hatia.
Polisi hiyo imesema kuwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti unatuma onyo kali kwa viongozi wakuu wa magenge kusitisha vitendo vya uhalifu vya ubakaji, utekaji nyara, na mauaji.
Soma pia:Vifo vya genge lenye silaha Haiti vyafikia 109
Innocent amewekewa vikwazo na Marekani, Umoja wa Ulaya na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, huku Marekani ikitoa zawadi ya dola milioni 2 kwa habari ztakazopelekea kukamatwa kwake. Amefunguliwa mashtaka nchini Marekani kwa utekaji nyara wa kutumia silaha wa wamisionari 16 wa Kikristo mnamo mwaka 2021 na kuuawa kwa mmishonari Marie Franklin na kutekwa nyara kwa mumewe mwaka 2022.