Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalishughulikia Makazi (UN-HABITAT) Bi.Anaclaudia Rossbach (kulia) akisisitiza jambo wakati wa kikao chake na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda mjini Zanzibar hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Makazi Duniani ( UN HABITAT) Anaclaudia Rossbach.
Viongozi hao walikutana hivi karibuni mjini Zanzibar katika kikao kilichohudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Bw. Deogratius Kalimenze, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya urasimishaji makazi Bw. Nicolaus Mwakasege pamoja na Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje Bw. Mbaraka Abdulrahman.
Katika mazungumzo yao. Mhe. Pinda alimueleza Mkurugenzi huyo wa UN-HABITAT kuwa, Tanzania inaunga mkono juhudi zinazofanywa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa katika kusaidia miradi mbalimbali nchini aliyoieleza kuwa imefikia takriban dola milioni 29.3.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa, ni uwepo wa miji salama na kuzuia uhalifu, maji na usafi wa mazingira, mfuko wa kuwezesha wanawake kumiliki ardhi pamoja na mradi wa usambazaji maji ziwa victoria ambapo ameielezea miradi hiyo yote kuwa imesaidia kuboresha maisha ya watanzania.
Aidha, amemueleza mkurugenzi huyo wa UN -HABITAT nia ya Serikali kulipatia shirika hilo ofisi hapa Tanzania ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ambapo Mkurugenzi huyo amekubali ombi la shirika lake kuwa na ofisi nchini Tanzania.
” tutaendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika miradi tofauti itakayoboresha makazi katika miji mbalimbali pamoja na mchakato mzima wa uanzishwaji ofisi ya UN-HABITAT Tanzania” alisema Anaclaudia.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalishughulikia Makazi (UN-HABITAT) Bi. Anaclaudia Rossbach ( wa nne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wengine mara baada ya kikao kilichofanyika mjini Zanzibar hivi karibuni.