Taswa Mwambao Marathon kufanyika Desemba 22 jijini Tanga

MBIO za TASWA Mwambao Marathon  zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), ambazo awali zilikuwa zifanyike mwishoni mwa mwezi uliopita sasa zitafanyika Desemba 22, 2024 jijini Tanga.

Siku moja kabla ya mbio hiyo kutafanyika Mkutano Mkuu wa TASWA asubuhi ya Desemba 21, 2024 jijini Tanga na baadaye mchana siku hiyo hiyo kutafanyika kongamano la kitaaluma kwa wanahabari za michezo kujadili masuala mbalimbali ikiwemo nafasi ya wanahabari kuelekea kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) za mwaka 2027 ambazo zifanyika kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Katibu Mkuu Msaidizi wa TASWA Imani Makongoro amesema kuwa  Mwambao Marathon 2024 ni mbio maalumu kuhamasisha wanamichezo na wananchi kwa ujumla kutumia  Nishati Safi ya Kupikia ili kutunza mazingira ikiwa na kauli mbiu ya kumtua mama kuni kichwani, hivyo katika kusukuma mbele ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka ya hadi kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia Nishati Safi ya Kupikia, Taswa itafanya mbio hii ambayo itakuwa endelevu kila mwaka, ikianzia Tanga mwaka huu na kisha itakuwa ikifanyika mikoa tofauti kila  mwaka.

TASWA inachukua fursa hii pia kuzishukuru Kampuni, Taasisi, Mashirika na wadau mbalimbali ambao wamejitokeza kuisapoti  Mbio hii kubwa ya kihistoria nchini iliyoandaliwa na Wanahabari  ikiunga mkono juhudi za Rais Samia katika matumizi na nishati safi.

Amesema kuwa Taswa inakaribisha  wadhamini zaidi kujitokeza, mashirika ya ndani na nje ya nchi, Taasisi, kampuni, watu binafsi, wadau wa mazingira na nishati safi ya kupikia kuendelea kujitokeza kushirikiana nasi kufanikisha mbio hii ambayo ni ya Kilometa 21, KM 10 na mbio za kujifurahisha (Fun Run) za KM 5. 

Wanaotaka kushiriki mbio hii wanatakiwa kujisajili kwa namba ya malipo ya Tigopesa 0777333110 jina TASWA Marathon kwa ada ya Sh 30,000.

Pia amesema kuwa kwa wanachama wa TASWA wanaotaka kushiriki Mkutano Mkuu wanatakiwa walipie ada ya uanachama ya mwaka mmoja ambayo ni Sh 30,000 kupitia benki ya CRDB, jina la akaunti Tanzania Sports Writers Association (TASWA), nambari ya akaunti ni 0133641150700 CRDB, mwisho wa kuthibitisha kushriki na kulipa ada ni Novemba 25, 2024.

Taswa Mwambao Marathoni ni tukio kubwa ambalo litahitimisha kalenda ya mwaka huu ya Taswa baada ya kufanya kwa mafanikio matukio mbalimbali ikiwamo la Media Day iliyofanyika Dar es Salaam Februari 10, 2024 ambayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  alikuwa mgeni Rasmi.

Related Posts