Wizara ya madini yadhamiria kurudisha minada ya ndani ya vito

Serikali kupitia Wizara ya Madini imeazimia kurudisha minada ya ndani ya madini ya vito itakayofanyika katika maeneo ya uzalishaji hususan Mirerani, Mahenge, Tunduru, Dar es salaam, Arusha na Tanga na kimataifa itafanyika mji wa Bangkok na Jaipur nchini Thailand.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 16, 2024 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini jijini Dodoma

Waziri Mavunde amesema kuwa baada ya taratibu za marekebisho ya kisheria kukamilika juu ya uendeshaji wa minada hiyo wanatarajia ndani ya muda mfupi ujao kuanza taraibu za kuweka miundombinu ya kuanza minada ya ndani.

Waziri Mavunde amefafanua kuwa, uendeshaji wa maonesho na minada ya kimataifa nchini ni fursa muhimu ya kutangaza madini ya vito yanayozalishwa hususan kwenye masoko ya kimataifa ambayo ni njia mojawapo ya kuwafikisha watanzania katika masoko ya uhakika na upatikanaji wa bei nzuri na stahiki.

Waziri Mavunde ameieleza Kamati ya Nishati na Madini kuwa, Mpango wa kurejesha minada ya madini ya vito ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha jijini Mwanza tarehe 13 Juni, 2024.

Kwa upande wake , Naibu Waziri wa madini Dkt.Steven Kiruswa amesema, kwa sasa wataalam wa Wizara ya Madini wamepata uzoefu mkubwa katika minada na maonesho ya kimataifa baada ya kujifunza namna biashara za kimataifa zinavyofanyika pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye mnyororo mzima wa thamani madini katika nchi mbalimbali ikiwemo Marekani , India , Afrika Kusini na Thailand.

Related Posts