Dodoma, 17 Oktoba 2024 – Benki mpya ya Ushirika ya Tanzania (CBT) imefanya Mkutano Mkuu wake wa Kwanza wa Mwaka (AGM) leo, ikiwa ni hatua muhimu katika maendeleo ya sekta ya ushirika nchini. Hatua hii inakuja ikiwa ni miezi michache baada ya muunganiko wa Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) na Benki ya Jamii ya Tandahimba (TACOBA), ambao ulikamilika tarehe 26 Mei 2024.
Kuanzishwa kwa benki hii ni ushahidi wa uongozi wa kimaono wa Abdulmajid Nsekela, Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), ambaye moja ya vipaumbele vyake baada ya kuteuliwana Rais Samia ilikuwa ni kuharakishamchakato wa uanzishwaji wa benki ya kitaifa ya ushirika.
Benki hiyo, ambayo sasa imesajiliwa rasmi na Benki Kuu ya Tanzania, inafanya kazi kama taasisi ya kibiashara inayohudumia sekta ya ushirika na soko kwa ujumla.
Tofauti na taasisi nyingine za kifedha zinazomilikiwa na serikali, CBT inamilikiwa kimsingi na vyama vya ushirika na wanachama wake (asilimia 51%), huku serikali ikishikilia hisa ya asilimia 10, na asilimia 39 iliyobaki inamilikiwa na watu binafsi na makampuni.
Hisa za ushirika zimehifadhiwa mahsusi kwa wanachama wa ushirika pekee, na zinaweza kuuzwa na kununuliwa miongoni mwao. CBT imejipanga kimkakati kuhudumia mnyororo mzima wa thamani wa biashara za ushirika, ikitoa huduma za kifedha zenye ushindani kwa lengo la kuwawezesha ushirika na kukuza ujumuishi wa kifedha.
Wakati wa mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, alipongeza mafanikio ya kuanzishwa kwa CBT, akihusisha mafanikio yake na umahiri wa uongozi wa Nsekela. “Kuzinduliwa kwa CBT ni mabadiliko makubwa kwa harakati za ushirika hapa Tanzania,” alibainisha.
Waziri huyo pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunga mkono hatua ya kuanzisha benki hiyo kwa kutoa Shilingi bilioni 5 na kuruhusu serikali kumiliki hisa ndani ya CBT.
Waziri Bashe alitangaza kuwa Rais Samia atazindua rasmi benki hiyo katika hafla kubwa hivi karibuni. Alihimiza vyama vyote vya ushirika vilivyo chini ya Wizara ya Kilimo kuchangamkia fursa ya benki hiyo kwa kufungua akaunti na kufanya biashara kupitia CBT.
Ili kuimarisha hili, alimwagiza Msajili wa Vyama vya Ushirika kuhakikisha kuwa miamala yote ya kilimo, kama vile mauzo ya korosho katika mikoa ya kusini, inasimamiwa kupitia CBT.
Pongezi za Waziri Bashe kwa CBT zinadhihirisha nafasi muhimu ambayo benki hiyo inatarajiwa kusimamia katika kuwezesha ushirika kote nchini. Wakati CBT ikiangazia kupanua wigo wake wa huduma, tayari inafanya kazi kupitia matawi yake ya Moshi na Tandahimba, huku tawi jipya likitarajiwa kufunguliwa Dodoma ifikapo Novemba na lingine Tabora kabla ya Desemba 2024.
Benki hiyo pia ina ushirikiano wa kimkakati na Benki ya CRDB, ambayo pia ni mwekezaji ndani ya CBT kwa asilimia 20, ikiruhusu wateja wa CBT kutumia mitandao ya ATM na mawakala wa CRDB Wakala nchi nzima wakati huu wa mpito.
Katika hotuba yake, Abdulmajid Nsekela, Mwenyekiti wa TCDC, alisisitiza dhamira yake ya kubadilisha mfumo wa ushirika wa Tanzania kuwa wenye ushindani, uaminifu, na manufaa kwa wanachama wake.
Alieleza furaha yake ya kuona muendelezo wa kukamilisha vipaumbele saba ambavyo bodi yake ilivianisha vinavyolenga kuboresha na kuimarisha sekta ya ushirika, huku kipaumbele kikubwa kikiwa ni mifumo ya kidijitali na uanzishwaji wa CBT. Mafanikio haya yanaenda sambamba na maono mapana ya Nsekela ya kuona ushirika ukiwa na uwezo wa kujitegemea na kuwa sehemu muhimu ya uchumi wa taifa.
Godfrey Ng’urah, Mkurugenzi Mtendaji wa CBT, alisisitiza dhamira ya benki hiyo kutoa suluhisho za kifedha za kibunifu zinazokidhi mahitaji ya vyama vya ushirika. Alieleza nafasi ya teknolojia katika mkakati wa CBT, lengo likiwa ni kuleta mapinduzi kwenye sekta ya ushirika kwa kuwezesha ushirika kufanya kazi kidijitali na kuongeza ujumuishaji wa kifedha kwa zaidi ya Watanzania milioni 10 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Ng’urah alibainisha lengo la CBT kufikia zaidi ya vyama 6,000 vya ushirika na kuhudumia zaidi ya wanachama milioni 8.
Akiunga mkono malengo haya, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CBT, Dk. Gervas Machimu, alieleza kuwa benki hiyo itafanya kazi kwa msingi wa benki ya watu wengi, ikitoa huduma nafuu na za ushindani zinazolenga kuongeza ujumuishaji wa kifedha kwa wakulima na ushirika. Benki hiyo pia inalenga kukuza uchumi kupitia uwekezaji wa kimkakati, miradi ya kitaifa, na fursa mbadala za kuzalisha kipato kwa vyama vya ushirika.
Matokeo ya kifedha ya CBT yanaonyesha mustakabali mzuri wa benki hiyo. Kulingana na taarifa ya kifedha iliyounganishwa ya benki hiyo, iliyotolewa tarehe 30 Septemba 2024, CBT ilipata faida halisi ya Shilingi milioni 646, huku jumla ya mikopo iliyotolewa ikiwa na thamani ya Shilingi bilioni 14.4. Amana za wateja zilifikia Shilingi bilioni 11.4, na mtaji wa wanahisa ulifikia Shilingi bilioni 52.
Kuanzishwa kwa CBT si tu ni mafanikio katika harakati za kuboresha ushirika nchini, bali pia ni hatua kubwa kuelekea ujumuishaji wa kifedha na uwezeshaji wa kiuchumi kwa mamilioni ya Watanzania. Kwa kutoa zana na rasilimali zinazohitajika na vyama vya ushirika ili viweze kufanikiwa, CBT inatarajiwa kuchukua nafasi muhimu katika sekta ya fedha nchini.
Mkutano Mkuu wa Mwaka ulimalizika kwa matumaini makubwa kutoka kwa wanahisa na wadau, ambao walionyesha imani katika uwezo wa CBT kutimiza malengo yake na kuleta mabadiliko ya kudumu kwenye sekta ya ushirika na uchumi wa Tanzania.