Gachagua atimuliwa wakati akiugua hospitali – DW – 18.10.2024

Baada ya siku mbili za kuwasilisha hoja na kuzifafanua, hatimaye Maseneta wamemtimua naibu wa rais Rigathi Gachagua. Maseneta wasiopungua 53 walipiga kura kumtimuakwa shtaka la kwanza kuhusu ushirika na kwamba wakenya wananufaika kwa kuzingatia mchango wao wa kisiasa. Kwa jumla maseneta walipiga kura iliyokubaliana na mashtaka 5 kati ya yote 11 yaliyomuandama.

Soma: Seneti ya Kenya kupiga kura kuamua hatma ya Gachagua

Kabla ya kura kupigwa, mawakili wa Rigathi Gachagua walioomba kikao kiahirishwe walijiondoa barazani baada ya maseneta kuridhia mchakato uendelee ijapokuwa mhusika mkuu hakuwako kujitetea.

Wakili kiongozi Paul Muite alilirai baraza la Senate kuwapa muda hadi Jumanne wiki ijayo ili mteja wao aweze kupata fursa ya kujitetea mbele yao.Hata hivyo kilio chake kiliambulia patupu na maseneta walipiga kura kuendelea na mchakato pasina uwepo wa naibu wa rais. 

Bunge la Kenya wakati wa kikao cha kujadili hoja ya kumwondoa madarakani Gachagua
Bunge la Kenya wakati wa kikao cha kujadili hoja ya kumwondoa madarakani GachaguaPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Gachagua aumwa na kulazwa Karen

Mchakato huo ulikwama kidogo pale naibu wa rais aliposhindwa kufika mbele ya baraza kujitetea baada ya kuumwa na kulazimika kulazwa kwenye hospitali ya Karen hapa jijini Nairobi. Kulingana na tabibu mkuu Dr Dan Gikonyo, naibu wa rais alipata maumivu makali ya kifua na ikamlazimu alazwe na ataendelea kuwa chini ya uangalizi Kwa saa 72 zijazo. Ijapokuwa ni haki ya naibu wa rais kujitetea mbele ya baraza , maseneta waliridhia kuendelea na mchakato bila uwepo wake. 

Soma kwa kina: Gachagua augua ghafla katikati mwa kesi yake mbele ya Seneti

Seneta Stewart Madzayo ni mwakilishi wa upinzani kwenye baraza la Senate na kwa mtazamo wake,” Senate inamtakia afueni ya haraka naibu wa rais na Mola amponye.Tuko kwenye njia panda ima tuendelee japo anaumwa au tumsubiri.” Ifahamike kuwa bunge la taifa limeandaa kikao maalum hii leo kujadili masuala mazito ya umma baada ya naibu wa rais kutimuliwa. Ijapokuwa naibu wa rais aliyechaguliwa na umma ametimuliwa, mrithi wake atachaguliwa na bunge la taifa.

Soma:Wabunge wa Kenya kupiga kura ya kumuondoa au la Gachagua

Rigathi Gachagua
Rigathi GachaguaPicha: Andrew Kasuku/AP/picture alliance

Itakumbukwa kuwa ,mbunge wa Kibwezi magharibi Mwengi Mutuse ndiye aliyewasilisha mswada wa kumtimua Rigathi Gachagua bungeni kwa mara ya kwanza tarehe 8 mwezi huu wa Oktoba.Seki Kanar ni seneta wa Kajiado na amesikitika kuwa ,”Naibu wa rais amehukumiwa akiwa anaumwa.Hakupata nafasi ya kujitetea na hiyo sio haki wala sawa.”

Mashtaka 11 ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka

Mbali na mashtaka ya kujilimbikia mali kwa njia zisizokuwa sawa, rais Gachagua alituhumiwa kwa kutumia watu wa kando kujipatia kandarasi ya vyandarua vya mbu vilivyotiwa dawa vya thamani ya shilingi bilioni 3.7 kupitia mamlaka ya ununuzi wa bidhaa za tiba, KEMSA.

Kulingana na mswada huo,naibu wa rais aliwashinikiza viongozi wa KEMSA kumpa kandarasi hiyo ya vyandarua vya mbu kutumia kampuni ya Crystal Ltd kinyume na utaratibu.Baraza la Seneti laanza kujadili hoja ya kuondolewa Gachagua

Hoja nyengine iliyoibuka ni kuwa naibu wa rais amekuwa akitoa kauli zinazoashiria kuwa wakenya wananufaika kwa kuzingatia mchango wao wa kisiasa kupitia vyama jambo ambalo limewakirihi wengi.

Kenya Nairobi | Mashujaa Day
Gachagua akiwa na rais Ruto siku ya Mashujaa 2022Picha: Simon Maina/AFP

Mashataka hayo pia yalijikita katika suala la naibu wa rais kujilimbikia mali kama vile hoteli ya kifahari ya Outspan,Olive Gardens na Treetops kwa kasi , hali inayoashiria kuwa kuna mkono wa ufisadi. Seneta wa Kirinyaga James Murango alihuzunika kuwa,” Fisi akitaka kumla mwanawe anasingizia kuwa ana harufu ya mbuzi.Sijaona ushahidi wowote unaomfanya naibu wa rais astahili kutimuliwa.Hana makosa yoyote.”

Mchakato unaofuata sasa ni wa kumteua mrithi wa naibu wa rais atakayehitaji ridhaa ya bunge la taifa.Kwa upande wake, Rigathi Gachagua ana kibarua cha kukimbilia mahakamani ili kulisafisha jina lake na kusaka uamuzi huo kubatilishwa. Hata hivyo milango ya kuwania nafasi ya uongozi wa umma imefungwa kikatiba.

 

Related Posts