Umoja wa Ulaya na Ghuba wakutana kujadili Gaza na Ukraine – DW – 17.10.2024

Viongozi wa Mataifa ya Ghuba ikiwa ni pamoja na Mwana mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman walikutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels katika mkutano wa kwanza wa kilele baina ya pande hizo siku ya Jumatano, kwa matumaini kwamba mazungumzo yao yanaweza kusaidia kupunguza kitisho kinacholetwa na kusambaa kwa machafuko kwenye eneo la Mashariki ya Kati. 

Mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya yanaangazia kufanya kazi kwa karibu zaidi na mataifa sita tajiri yaliyopo kwenye Baraza la Ushirikiano la Mataifa ya Ghuba, GCC, hasa katika mizozo ya Mashariki ya Kati na Ukraine. Mataifa hayo ni Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell aliwaambia waandishi wa habari jana usiku kwamba kipaumbele cha pamoja ni usitishwaji wa haraka na endelevu wa mapigano, kuachiliwa mateka na ufikishwaji kamili wa misaada ya kiutu kwa raia wa Ukanda wa Gaza.

”Na kwa Lebanon, wito wetu ni  kusitishwa mapigano mara moja na utekelezwaji wa makubaliano. Azimio namba 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliungwa mkono na wengi kwenye mkutano huo na pia tunalaani vikali mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, UNIFIL,” alisema Borrell.

Mkutano wa kilele kati ya GCC na EU mjini Brüssels
Emir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani(kushoto) akizungumza na Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel kwenye mkutano wa kilele kati ya mataifa ya Ghuba na umoja huo, Oktoba 17.10.2024Picha: Virginia Mayo/dpa/AP/picture alliance

Qatar yarejesha hoja ya “suluhu ya mataifa mawili”

Emir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani kwa upande wake alisema mazungumzo yao kwa kiasi kikubwa yalijikita katika masuala hayo na kusema pamoja na yote, bado wanaamini kwamba suluhu ya kudumu katika mzozo wa Mashariki ya Kati ni ile iliyotajwa kwa muda mrefu ya mataifa mawili.

Alisema ”Tulichoona katika mijadala yote hii ni kwamba nchi nyingi zinakubaliana kimsingi kwamba njia pekee ya kusonga mbele kwenye mizozo ya Mashariki ya Kati ni kutekeleza suluhisho la mataifa mawili. Na pia kusitishwa mapigano na kuvimaliza vita hivi  mara moja.”

Amesema wanatumai kwamba mkutano huu wa kwanza utakuwa ni hatua ya mwanzo ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria kati ya GCC na Umoja wa Ulaya.

Mohammed bin Salman akikaribishwa kwenye mkutano mjini Brüssels
Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen akiwa na Mwanamfalme Mohammed bin Salman bin Abdulaziz Al Saud(katikati) na Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel katika mkutano wa kilele kati ya mataifa ya Ghuba na Umoja wa UlayaPicha: Johanna Geron/REUTERS

Matamshi yake yaliungwa mkono na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen aliyeliambia kusanyiko hilo kwamba ipo haja ya kufanya kila lililo ndani ya uwezo wao na kuhamasisha juhudi za kidiplomasia kuzuia kitisho cha kusambaa zaidi kwa mzozo huo.

Masuala zaidi yalijadiliwa kwenye mkutano wa EU-GCC

Masuala mengine yaliyojadiliwa yalihusu nishati na mabadiliko ya tabianchi.

Kulingana na Borrell, pande hizo pia zimekubaliana kuongeza kasi ya kufikia makubaliano ya biashara huria yaliyochukua muda mrefu.

Hata hivyo, msukumo wa mataifa hayo ya Ghuba yanayotaka umoja huo uwaruhusu raia wao kuingia kwenye eneo la Schengen bila ya malipo, haukuzaa matunda.

Na kuhusu vita vya Urusi na Ukraine, ingawa kulikuwa na mitazamo tofauti na hususan kuelekea utekelezwaji wa vikwazo vya Magharibi na msukumo wa Umoja wa Ulaya kuiadhibu Iran kwa kuisaidia Urusi katika vita hivyo, lakini bado kumeonekana matumaini ya kushirikiana kwa karibu.

Taarifa ya pamoja baada ya mkutano huo ilirejelea kwa mapana ahadi ya pande hizo kuhakikisha “heshima, ulinzi na uendelezaji wa haki za binadamu kwa wote”.

Related Posts