NAIBU Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi, ameitaka Taasisi simamizi za Maadili na Mamlaka simamizi za Maadili kuzingatia waraka wa utumishi wa umma Na. 6 wa mwaka 2020 kuhusu mavazi ya watumishi wa umma.
Akizungumza wakati wa kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora, Daudi alisema kuwa ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu hali isiyoridhisha ya mavazi ya watumishi.
Aidha aliendelea kusema kuwa ofisi imeanza kupokea tuhuma za mmomonyoko wa maadili, ikiwemo vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, vinavyokiuka mila na desturi za nchi.
Pamoja na hayo alitaka kikao hicho kijadili hatua stahiki za kudhibiti vitendo hivyo na kuboresha maadili katika utumishi wa umma.
” Mawasilisho yenu na majadiliano yenu, yawaongoze kwenye ubunifu wa mikakati ya kuboresha misingi ya maadili ya utendaji na maadili ya kitaaluma kama njia mojawapo ya kuimarisha utoaji wa huduma katika Utumishi wa Umma na kuleta ustawi kwa wananchi”. Alisema Daudi
Daudi pia alihimiza matumizi ya teknolojia, hasa Serikali Mtandao, katika kubaini na kudhibiti uvunjifu wa maadili.
Aliongeza kuwa mawasiliano na majadiliano yatasaidia kubuni mikakati bora ya kuimarisha maadili na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili, Ally Ngowo, alieleza kuwa matarajio ya kikao hicho ni kupokea taarifa za utekelezaji wa masuala ya maadili kutoka kwa taasisi mbalimbali, huku akisisitiza umuhimu wa mfumo wa e-Mrejesho katika usimamizi wa maadili.
“Matarajio yetu ni kuwa tutapokea taarifa za utekelezaji kutoka kwa taasisi pamoja na mamlaka ya usimamizi za maadili ya kitaaluma,taarifa za utekelezaji ni za kipindi cha kuanzia mwezi Septemba 2023 ambapo ndio kikao chetu cha mwisho hadi kufikia Septemba 2024”. Alisema
Katika kikao hiki moja Taasisi zitakazotoa Taarifa ya utekelezaji wa Usimamaizi wa Maadili kutoka maeneo yao ya kazi ni pamoja na OR-IKULU,OR-MUUUB,TAKUKURU na zinginezo kwa mwezi September 2023 hadi Septemba 2024.